đź“Ś Awataka waumini kushirikiana na Askofu Pangani
đź“ŚSerikali kuendelea kushirikiana na taasisi za dini nchini
đź“Ś Rais Samia apewa tuzo kwa uongozi uliotukuka na kulinda amani
*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kudumisha amani, mshikamano na upendo na kamwe wasigawanywe kwa sababu yoyote.
Amesema hayo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuwekwa wakfu Askofu Robert Yondam Pangani wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi iliyofanyika leo Juni 2, 2024 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji mkoani Mbeya.
“Nimefurahi kusikia wewe ni mtu mtulivu na myenyenyekevu sana upokee jambo hili kwa amani, nina imani eneo lako la mahubiri litakuwa kubwa zaidi na sisi tutaendelea kukuombea kwa Mungu ili lile aliloweka ndani yako liweze kujitokeza”, amesema Dkt. Biteko.
Ametoa wito “Waumini wenzangu huyu si malaika ni binadamu itafika wakati atachoka naomba mumtie moyo, na msiache kumuombea na kumtii inawezekana kuna anayejua kuliko yeye lakini yeye amepewa fursa ya kuwaongoza nyinyi hivyo mumtii. Pia tusibaguane kwa dini zetu au vyama vyetu vya siasa, sisi tuliokaa hapa hatujatambuana kwa makabila yetu tunatambuana kwa utanzania wetu, wakati wote muhubiri amani na mtu yeyote mwenye shida aone Tanzania ni mahali salama” .
Pia, amemsii Askofu Pangani kuwasikiliza watangulizi wake pamoja na Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania kwa kuwa wana heshima na hekima.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera amesema kuwa Mhe.Rais Samia ameunganisha taasisi za dini na alichangia milioni 50 katika Kanisa la Moravian kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mkoani Dodoma.
“ Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati naomba utusaidie katika mgogoro wa kiwanja mkoani Dodoma ili waweze kujenga ofisi zao, Rais Samia yuko pamoja nao na ameunganisha taasisi za dini na ukiona taasisi hizi ziko pamoja ni jitihada zake hasa hapa Mbeya”, amesema Mhe. Homera.
Naye, Askofu Robert Yondam Pangani amesema kuwa amepokea kwa heshima na kwa unyenyekevu mkubwa nafasi aliyopewa na anaahidi kuungana na viongozi wa dini kuhakikisha amani inadumu pamoja na kuimarisha ushirikiano na Serikali.
Askofu Pangani ametaja shughuli mbalinbali zinazofanywa na Kanisa hilo la Moravian Jimbo la Kusini Magharibi ikiwemo kuwa na miradi inayotoa ajira kwa vijana na kutunza watoto yatima sambamba na kuwasomesha katika ngazi mbalimbali za elimu kuanzia awali, shule za msingi hadi vyuo vikuu.
“Watu 1,203 wenye mahitaji maalum wameendelea kupatiwa mahitaji mbalimbali na Kanisa ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa wajasiriamali, Kanisa pia linaungana Serikali katika utunzaji wa mazingira ili kutunza vyanzo vyetu vya maji na kutatua changamoto ya maji kama ambavyo Rais wetu amedhamiria kumtua mama ndoo kichwani”, amesema Askofu Pangani.
Amesisitiza “Nampongeza Mhe. Rais Samia kwa mambo muhimu anayoendelea kufanya katika Taifa hili la kulinda amani pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali ya maji, barabara na umeme ambao uko nchi nzima mijini na vijini, na mimi naahidi kuwa Kanisa litaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na tutaendelea kuwaombea viongozi wetu”.
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Kanisa la Moravian Duniani, Mchungaji Erord Rupia Simae wakati akisoma barua ya salamu kutoka kwa Rais wa Moravian Duniani, amesema kuwa wanampongeza Askofu Robert Yondam Pangani kwa kupata fursa ya kuongeza Kanisa hilo katika Jimbo la Kusini Magharibi na kuwa yeye ni mchungaji aliyepewa namba 380 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo duniani mwaka 1457 na pia amepewa namba 318 tangu Kanisa hilo kufanywa upya mwaka 1727.
Awali, Askofu Ezekiel Yona akimzungumzia
Askofu Robert Yondam Pangani amesema kuwa amepewa nafasi na heshima hiyo na Mungu hivyo akatende haki katika kutekeleza majukumu yake kwa kuwa watu wanataka kuona Askofu anayewarudisha watu kwa bwana na kuponya mioyo yao.
“Lazima tumtangulize Mungu ndani ya Ofisi ya Baba Askofu na kwa kuwa wewe umepitia ngazi nyingi katika kanisa hivyo kwa sasa unalijua kanisa vizuri zaidi ndani na nje. Ofisi yako ndio ya kujenga kanisa la kuabudu ndio na kweli”, amesisitiza Askofu Yona
Ameongeza kuwa Jimbo la Kusini Magharibi ni jimbo kubwa katika majimbo ya Kanisa la Moravian duniani na hivyo ashughulike nalo huku akiwaomba waamini wa kanisa hilo kutoa ushirikiano kwa Askofu huyo.
Pamoja na hayo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amepanda mti katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji kilichopo Mbeya ikiwa ni kumbukumbu ya ushiriki wake katika ibada hiyo.
Pia katika ibada hiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepewa tuzo maalum ya utumishi uliotukuka, viongozi wengine waliopewa tuzo za utumishi uliotukuka pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, Spika wa Bunge na Rais wa Mabunge Duniani, Mhe. Tulia Ackson na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera.
Aidha, tendo la kumweka wakfu Askofu Robert Yondam Pangani limeongozwa na Askofu Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania, Conrad Nguvumali Sikombe pamoja na maaskofu wengine wa Kanisa hilo. Ibada hiyo pia imehudhuriwa na maaskofu kutoka nchi za Uingereza na Zambia.