Featured Kitaifa

RAIS SAMIA NA RAIS YOON SUK YEOL WASHUHUDIA UTIAJI SAINI WA MIKATABA

Written by mzalendo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Yoon Suk Yeol wakati wakishuhudia Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na Waziri wa Biashara wa Korea Inkyo Cheong wakisaini Tamko la Pamoja kuhusu Uanzishwaji wa Majadiliano juu ya Mkataba wa Ushirikiano Kiuchumi. Hafla ya utiaji saini imefanyika katika Ikulu nchini humo tarehe 02 Juni, 2024.

………

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais Yoon Suk Yeol wa Jamhuri ya Korea wameshuhudia utiaji saini wa Mkataba mmoja, Hati za Makubaliano (MOU) 2 na Tamko la Pamoja la kuanzisha Mkataba wa Ushirikiano wa Uchumi (EPA).

Mkataba huu utaiwezesha Tanzania kupokea mkopo kutoka Korea wa kiasi cha Dola za Kimarekani Bilioni 2.5 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia (2024- 2028). 

Fedha hizo kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya maendeleo zinatolewa chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi wa Serikali ya Korea (EDCF).

Ili kufungua milango zaidi ya ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi, Tanzania na Korea zimesaini pia mkataba wa EPA utakaowezesha kuufanya uhusiano kuwa wa kimkakati hususan katika Nyanja za Biashara, Uwekezaji, Viwanda, Usafirishaji nakadhalika.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 3 tu barani Afrika ambazo zitafanya majadiliano hayo yatakayozaa Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Korea. Nchi zingine ni Morocco na Kenya.

Hati za Makubaliano zilizotiwa saini leo ni pamoja na Ushirikiano katika Uchumi wa Buluu ambapo Tanzania itashirikiana na Korea Kusini katika maeneo ya uvuvi, viwanda vya kuchakata mazao ya bahari, ujenzi wa bandari za uvuvi, teknolojia na tafiti za masuala ya bahari. 

Vile vile, Wizara ya Madini ya Tanzania na Wizara ya Biashara, Viwanda na Nishati ya Korea Kusini zimetia saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Madini ya Kimkakati.  

Tanzania na Korea Kusini zitashirikiana katika utafiti, uwekezaji, uchimbaji na kujenga uwezo wa kuongeza thamani ya madini ya kimkakati nchini Tanzania. Madini hayo ni Nickel, Lithium na Kinywe.

Wakati huo huo, Rais Samia amependekeza ushirikiano wa sekta nyingine mpya zikiwemo maendeleo ya nishati ya gesi asilia; sekta ya Ubunifu ikiwemo sanaa na filamu; na kufunguliwa kwa soko la ajira la nchini Korea kwa vijana wa Tanzania kupitia mpango wa Employment Permit System (EPS).

Rais Samia amehitimisha ziara rasmi ya siku mbili 2, na anatarajia kuanza ziara ya kikazi ambapo atahudhuria mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Korea na Afrika.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Yoon Suk Yeol wakati wakishuhudia Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na Waziri wa Biashara wa Korea Inkyo Cheong wakisaini Tamko la Pamoja kuhusu Uanzishwaji wa Majadiliano juu ya Mkataba wa Ushirikiano Kiuchumi. Hafla ya utiaji saini imefanyika katika Ikulu nchini humo tarehe 02 Juni, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Yoon Suk Yeol wakati wakishuhudia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi na Fedha (Jamhuri ya Korea) Choi Sang Mok wakisaini Mkataba wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Korea kuhusu Mkopo unaotolewa na Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi wa Serikali ya Korea (Economic Development Cooperation Fund-EDCF). Hafla ya utiaji saini imefanyika katika Ikulu nchini humo tarehe 02 Juni, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Yoon Suk Yeol wakati wakishuhudia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba pamoja na Waziri wa Biashara wa Korea Inkyo Cheong wakibadilishana Hati ya Makubaliano kati ya Wizara ya Madini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Biashara, Viwanda na Nishati ya Jamhuri ya Korea kuhusu Ushirikiano katika Madini ya Kimkakati. Hafla ya utiaji saini imefanyika katika Ikulu nchini humo tarehe 02 Juni, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Korea Mhe. Yoon Suk Yeol wakati wakishuhudia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba pamoja na Waziri wa Uvuvi na masuala ya Bahari kutoka Jamhuri ya Korea Kang Do-Hyung wakisaini Hati baina ya nchi mbili kuhusu Ushirikiano katika maendeleo ya Uchumi wa Buluu. Hafla ya utiaji saini imefanyika katika Ikulu nchini humo tarehe 02 Juni, 2024.

About the author

mzalendo