Na Gideon Gregory, Dodoma.
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amekemea
taarifa za kupotosha zinazotolewa na vyombo vya habari kuhusu vivuko vya Kigamboni na kuzua taharuki kwa wananchi wa eneo hilo.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Mei 29,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha ujao 2024/25 na kuongeza kuwa Serikali ipo kazini na haiwezi kuhatarisha usalama wa raia wake kwa namna yoyote ile.
“Hivyo, niwaombe wananchi wa Kigamboni kuwa watulivu wakati Serikali inaendelea kuboresha huduma za vivuko pale Kigamboni, sambamba na maboresho ya barabara ya Kibada – Mwasonga Jct na Songani Jct – Kijata Jct yanayolenga kuifanya Kigamboni kuwa mji bora.
Pia Waziri Bashungwa amezungumzia kuhusu suala la kukabiliana na changamoto ya kuharibika kwa barabara kabla ya muda wake ambapo amesema Wizara imepanga kuanza kutumia mitambo maalum ya kupima ubora wa barabara (Road Scanners).
Amesema matumizi ya teknolojia hiyo yatawawezesha kupima ubora wa barabara kama X– ray inavyopima mwili wa binadamu.
“Wizara imeamua kutumia teknolojia hii ya kisasa ili kuondoa kabisa matumizi ya vifaa visivyostahili katika upimaji wa ubora wa barabara vinavyotumika kwa sasa, hivyo sururu sasa basi”, amesema.
Pia amesena Matumizi ya mitambo hiyo
yatadhibiti makandarasi wasio waaminifu wanaocheza na viwango vya ubora wa barabara wanazojenga.
“Mitambo iliyonunuliwa ina thamani ya Shilingi bilioni 5.1. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kununua mitambo hii”, amesema.