Featured Kitaifa

TEKNOLOJIA MBADALA KUIMARISHA MTANDAO WA BARABARA NCHINI

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Teknolojia mbadala kuimarisha mtandao wa barabara ikiwemo ujenzi wa madaraja imara na madhubuti itaendelea kutumiwa nchini na Wakala ya Barabara za Vijijini na Vijijini – TARURA.

Yameelezwa hayo na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila mbele ya waandishi wa habari katika banda la maonesho ya TARURA kwenye mkutano wa 30 wa wahandisi Afrika.

“TARURA wanaonesha utaalamu wanafanya ikiwemo ujenzi wa ‘structure’ mbalimbali za kupitishia maji, wanajenga kwa mawe teknolojia ambayo inapunguza gharama,” amesema.

Akizungumza namna Serikali ilivyojipanga kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na mvua zilizoanza kunyesha tangu Oktoba, 2023 na zinazoendelea hadi sasa, Naibu Katibu Mkuu Mativila amebainisha kwamba bado kuna sehemu nyingi mvua zinaendelea kunyesha, miundombinu mingi imeharibika, mvua zilizokuja hazikuwa za kawaida kama miaka mingine.

Hata hivyo amesema wameshafanya tathimini na zinahitaji kiasi cha Tsh. Bil. 2 kurejeresha miundombinu iliyoharibiwa na mvua na Serikali ipo tayari kutoa fedha hizo

Naye, Msimamizi wa Teknolojia Mbadala TARURA – Makao Makuu Mhandisi Mshauri Pharels Ngeleja amesema tayari wamejenga madaraja 256 kwa teknolojia ya mawe yaliyogharimu Tsh. Bil. 13.

“Teknolojia ya mawe tunatumia pia kujenga barabara, kuna Km. 26.18 zimekamilika Mkoani Mwanza, Kigoma na Rukwa, pia kwenye barabara zetu zingine tunatumia teknolojia za Ecoroad, Ecozyme na Polymer”.

“Tumejenga barabara ya Sawala Km. 13 Mkoani Iringa, Chamwino – Dodoma pia tunaendelea na hizi teknolojia, Dodoma kuna barabara inaitwa daraja dogo tumekamilisha.Miradi hii ipo maeneo mbalimbali ambapo tunaendelea,” amesema Mhandisi Ngereja.

Vilevile amesema TARURA kupitia kitengo cha mambo ya mazingira wanaendelea pia kufuatilia kwa ukaribu athari za mabadiliko ya tabia nchi ili kujiimarisha zaidi katika ujenzi wa miundombinu yake.

TARURA imeweza kujenga barabara kwa kutumia teknolojia ya Ecoroad, Ecozyme na Polymer katika barabara ya Chamwino Km. 7,Itilima Km. 5, Sawala-Mkonge Km. 10 na Daraja dogo -Dodoma Km.1.

About the author

mzalendo