Featured Kitaifa

MABADILIKO YA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU NI SEHEMU MUHIMU YA UTAWALA BORA

Written by mzalendo

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Mhe. Dkt. Festo Dugange (Mb) amesema Serikali inatambua kuwa, mabadiliko ya Sheria, Kanuni na Taratibu ni sehemu muhimu ya utawala bora na maendeleo endelevu ya jamii.

Dkt.Dugange amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu wakati akijibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, Mbunge wa Viti Maalum aliyeuliza Je, lini Serikali itarekebisha utaratibu wa Naibu Meya na Naibu Wenyeviti wa Halmashauri Kuhudumu Miaka Mitano badala ya kuchaguliwa kila mwaka?

“Kanuni za Kudumu za Halmashauri za Wilaya zinazoelezea uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti zimetungwa chini ya kifungu cha 70(1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 287 na Kanuni za Kudumu za Halmashauri za Miji zinazoelezea Uchaguzi wa Naibu Meya zimetungwa chini ya kifungu cha 42 (1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 288. Hata hivyo, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ikipokea hoja kutoka kwa wadau walio wengi kuhusu hitaji la mabadiliko ya Kanuni hizi itafanyia kazi.” Mhe. Dkt Dugange.

Amesema sheria zilizopo zinaelekeza uchaguzi wa Makamo Mwenyekiti wa Halmashauri na Naibu Meya kila mwaka lakini kuna Halmashauri nyingi  ambazo Manaibu Meya na Makamo wa Wenyeviti hudumu kwa muda wa miaka Mitano.

About the author

mzalendo