Featured Kitaifa

WIZARA YA UJENZI IMEJIPANGA KURUDISHA MIUNDOMBINU ILIYOHARIBIKA: BASHUNGWA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema wizara kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imejipanga kufanya matengenezo makubwa kwa lengo la kurudisha mawasiliano kwenye barabara, madaraja, makalvati pamoja na vivuko zilizokatika kutokana na mvua za El-Nino.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) leo tarehe 28 Mei 2024 kwenye maonesho ya wizara na taasisi zake, Bashungwa amesema kuwa mvua kubwa iliyonyesha hali kadhalika Kimbunga Hidaya vimeathiri miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema katika mwaka wa fedha 2023/24, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha majenzi ya Barabara na madaraja sambamba na ukarabati wa vivuko na ujenzi wa vivuko vipya.

Bashungwa amesema kuwa katika miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia madarakani miradi ya barabara 25 imekamilika yenye urefu wa kilomita 1,198 huku miradi 74 ya barabara ikiwa katika hatua mbalimbali ya utekelezaji.

“Tulikuwa tunaenda vizuri sana kwenye majenzi ya barabara mpaka pale nchi ilipokumbwa na mvua kubwa za El-Nino ambazo zimeleta athari kubwa ya kuharibika kwa barabara.”amesema.

Aidha, Bashungwa amesema kutokana na uharibifu huo, Serikali imeelekeza baadhi ya fedha ambazo zilikuwa ziendelee kujenga barabara kwa kiwango cha lami kuzipeleka kwenye fedha za dharura ili kurejesha mawasiliano kwenye barabara zilizokatika.

Pia, amesema baadhi ya fedha ambazo zingeendelea kutumika kujenga barabara za kiwango cha tabaka la lami kwenye fedha za dharura kwa ajili ya kurudisha mawasiliano kwa barabara ambazo zimekuwa zimekatika na kutokuwa na mawasiliano.

“Mvua zitakapoisha tunajipanga kufanya matengenezo makubwa kurudisha barabara zile ambazo zimeharibika, kwa hiyo sehemu ya bajeti ambayo tunakwenda kuiwasilisha bungeni kesho itakuwa na sehemu ya kurudisha barabara ambazo zimeharibika sana.”

About the author

mzalendoeditor