Featured Kitaifa

TUSHIRIKIANE KWA PAMOJA KUTOKOMEZA SARATANI

Written by mzalendoeditor

Na. WAF – Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau ikiwemo Taasisi ya Shujaa cancer Foundation katika kutokomeza ugonjwa wa Saratani pamoja na kuelimisha jamii kwa kuwa ugonjwa huo unatibika ukigundulika mapema.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Aprili 18, 2024 kwenye kikao na Mkurugenzi wa ‘Shujaa Cancer Foundation’ Bi. Glory Kida aliyeambatana na Mkurugenzi wa Mipango wa Shujaa Cancer Foundation Bi. Kisa Mwakatobe katika ofisi yake Mkoani Dodoma.

“Tutaendelea kushirikiana na wadau wetu katika Sekta ya Afya ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi ili kwa pamoja tuweze kutokomeza ugonjwa wa Saratani kwa kuwa ugonjwa huo umekua ukiongezeka kutokana na wananchi kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya ugonjwa huo.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amewaelekeza watalaam wa Wizara ya Afya kukaa pamoja na mashujaa kwa ajili ya kuandaa mikakati ya pamoja katika udhibiti wa ugonjwa wa Saratani hususani Saratani ya Mlango wa Kizazi, Tezi dume pamoja na Saratani ya Matiti ambazo ndio zinaongoza hapa nchini.

Waziri Ummy amefarijika kuona uwepo wa watu wanaoishi muda mrefu baada ya kupata matibabu ya Saratani, Taasisi hiyo imeonesha uwepo wa wajumbe wake ambao wamekuwa wakiishi kwa zaidi ya miaka 22 baada ya kupona ugonjwa huo na hivyo kushiriki katika kuelimisha jamii ili kuondoa imani potofu kuwa Saratani haitibiki na kuondoa hofu miongoni mwa jamii kuhusu kuanza matibabu ya ugonjwa huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ‘Shujaa Cancer Foundation’ Bi. Glory Kida ameshukuru juhudi za Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kupanua huduma za chanjo kwa wasichana walio na umri wa miaka 14 pamoja na kuimarisha huduma za uchunguzi hapa nchini.

Mwisho, Waziri Ummy amepokea zawadi kutoka kwa Bi Glory aliyeambatana na Bi. Kisa iliyotolewa na ‘Africa Cervical Health Alliance’ (ACHA) ambayo ni shirikisho la vyama vinavyolenga kutokomeza tatizo la Saratani barani Afrika ambapo Tanzania ni mjumbe kwenye umoja huo.

About the author

mzalendoeditor