Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Mkoa na Halmashauri ya CCM mkoa wa Dodoma Ndg. Halima White akizungumza na wananchi wa Iloje, Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Na Gideon Gregory, Dodoma.
Wananchi wa Kata ya Loje Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma wamesema ukosefu wa shule ya Sekondari maeneo ya karibu na maeneo yao kumepelekea baadhi ya wazazi kuwaachisha watoto wao masomo na kuwaruhusu kwenda kufanya kazi katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Mjini licha ya wao kuanza na ujenzi wa madarasa mawili na Ofisi moja.
Wananchi wameyasema hayo baada ya Jumuiya ya umoja wa wazazi Tanzania ilipotembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali pamoja na kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Akijibia baadhi ya Changamoto hizo Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Mkoa na Halmashauri ya CCM mkoa wa Dodoma Ndg. Halima White amesema changamoto ya shule wataenda kuifanyia kazi ili kuhakikisha mwakani wanakuwa na shule ya Sekondari katika kata hiyo.
“Nimeridhishwa na juhudi zenu wananchi wa Kata ya Loje na kwakuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia ni sikivu naomba niwaambie kwamba mpaka kufikia mwakani nayie mtakuwa na shule yenu hapa pia hautegemei sasa kuona watoto hawaendi wala wanaachishwa shule,”amesema.
Sanjari na hayo Ndg. Halima ameonesha kutoridhishwa na mradi wa barabara unaotelezwa na TASAF kwani upo chini ya kiwango na kumuagiza diwani wa kata pamoja na viongozi wa chama kusimamia vyema ujenzi huo.
Kwa upande wake Katibu Elimu, Malezi na Mazingira Wialaya ya Chamwino Bi. Hilda Kadunda akisoma taarifa fupi ya maadhimisho ya wiki ya Umoja wa wazazi Wilayani humo amewahimiza wazazi/ walezi pamoja na wanafunzi kuzingatia umuhimu wa Elimu kwani ndiyo ufunguo wa maisha.
“Jumuiya inaendelea kuihimiza Serikali kuelendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia ili iwe chachu ya utoaji wa elimu bora kwa wananchi,”amesema.