Featured Kitaifa

CCM YALAANI BENDERA YAKE KUTUMIKA KWENYE USAFIRISHAJI WA WAHAMIAJI HARAMU

Written by mzalendo

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, John Nzwalile amelaani kitendo cha watuhumiwa wa usafirishaji wahamiaji haramu kutumia bendera ya chama hicho kufanyia uhalifu.

Awali, Polisi mkoani Manyara imeeleza kumshikilia Edward Erihard, mkazi wa Mkoa wa Dodoma akituhumiwa kusafirisha wahamiaji haramu 20 raia wa Ethiopia.

Erihard (31), anadaiwa kuendesha gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 akiwa amewabeba wahamiaji hao.

Gari hilo linadaiwa lilikuwa linapeperusha bendera ya CCM, lengo lilikuwa kuonyesha kuna kiongozi wa chama hicho anasafiri.

“CCM ni chama makini kinachojali uadilifu, hivyo vyombo husika vichukue hatua kali kwa wote waliohusika katika tukio hilo la kutumia bendera yetu na kufanya uhalifu,” amesema Nzwalile.

Amedai watuhumiwa wametumia bendera ya CCM kuweka kwenye gari ili kufanya uhalifu na kukichafua chama hicho jambo ambalo haliwezekani hata kama lingekuwa gari la chama hicho.

“Tunatoa wito kwa vyombo husika kuwachukulia hatua kali wahusika ikiwamo kuwafikisha mahakamani ili washtakiwe kwa kosa walilolifanya,” amesema Nzwalile.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Lucas Mwakatundu akizungumza na Mwananchi Digital, Machi 25, 2024 amesema tukio hilo limetokea Minjingu wilayani Babati, jioni ya Machi 23, 2024.

Mwakatundu amedai gari hilo wamelikamata katika kizuizi kilichopo Barabara ya Arusha kwenda Babati eneo la Minjingu likiwa na wahamiaji haramu 20 raia wa Ethiopia.

Amedai wahamiaji hao walikuwa wakisafirishwa kwa kutumia gari lenye namba za usajili T.774 BDL aina ya Toyota Land Cruiser likiwa na bendera ya CCM.

Amesema askari wa usalama barabarani walilisimamisha gari hilo na baada ya upekuzi waliona sura tofauti na Watanzania ikabidi liegeshwe pembeni.

Kaimu Kamanda Mwakatundu amedai baada ya kuwashusha ndipo walipobaini walikuwapo wahamiaji haramu 20.

#REPOST MWANANCHI.

About the author

mzalendo