RAIS Vladimir Putin amepata pigo la kwanza tangu vita yake na Ukraine ianze baada ya Mshauri wake Mkuu Bw.Anatoly Chubais kutangaza kujiuzulu wadhifa wake wa uwakilishi wa kimataifa.
Chubais anakuwa ofisa wa kwanza kujiuzulu katika serikali ya Putin tangu atangaze vita dhidi ya Ukraine ambapo hatua hiyo imekuja baada ya kile kinachosadikika kuwa ni kutokukubaliana na mauaji yanayotekelezwa na Rais Putin nchini Ukraine.
Shirika la Habari la TASS la nchini Urusi, limemnukuu Msemaji Mkuu wa Ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov akithibitisha kujiuzulu kwa afisa huyo na kueleza kwamba amechukua uamuzi huo kwa hiyari yake mwenyewe:
“Ndiyo, Chubais amejiuzulu kwa hiari yake mwenyewe, kama ameshaondoka Urusi au bado yupo hiyo ni juu yake mwenyewe.”
Taarifa zinasema Chubais alitangaza kujiuzulu kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook akiwa pamoja na mke wake nchini Uturuki.
Duru za kiintelijensia zinasema Chubais amekuwa ni mtu wa kupinga maamuzi ya Rais Putin tangu awali kwani baada ya vita kuanza, kupitia ukurasa wake wa Facebook aliweka picha ya mauaji ya kiongozi wa upinzani, Boris Nemtsov katika maadhimisho ya siku ya kifo chake.
Pamoja na kwamba Chubais amejiuzulu lakini hajafafanua ni sababu ipi imemfanya ajiuzulu.
Kiongozi huyu mkongwe alipata umaarufu mkubwa baada ya kupigania mabadiliko na kukua kwa uchumi wa Urusi miaka ya 1990 mara baada ya kuanguka kwa utawala wa kisovieti.
Viongozi wa vyama vya upinzani nchini Urusi wameonesha kutoridhishwa na kitendo cha Chubais kujiuzulu akiwemo msemaji wa mwanasiasa na mpinzani mkubwa wa Putin ambaye kwa sasa yupo jela, Alexei Navalny, Kira Yarmysh.
Yarmysh amenukuliwa akisema kujiuzulu kwa Chubais ni kwa sababu ya kupinga vita wala si kwa sababu ya hofu juu ya usalama wake au hofu juu ya fedha zake.
Kwa upande mwingine, Mshauri wa Rais wa Ukraine, Mykhaylo Podolyak alisema kuwa inashangaza kuona viongozi wawili wakubwa wa usalama wa Urusi hawaonekani na hawajulikani walipo.
Aliwataja Waziri wa Ulinzi, Sergie Shoigu na Mnadhimu wa Jeshi Valery Gerasimov wakiwa pamoja na mkuu wa idara ya siri wa Urusi kwamba hawafahamiki walipo, jambo linalotia shaka juu ya hali ya kidiplomasia ndani ya Urusi.
Wimbi la kujiuzulu linaendelea baada ya hivi karibuni mwandishi wa habari na mhariri wa kituo cha televisheni cha Channel One, Marina Ovsyannikova kujiuzulu.
CHANZO:GLOBAL TV