Featured Kitaifa

WAFANYABIASHARA WAZAWA MKOANI MARA WAENDELEA KUNUFAIKA NA MAFUNZO KUPITIA PROGRAMU YA KUWAJENGEA UWEZO YA BARRICK NORTH MARA

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rorya, Juma Chikoka, aliyekuwa Mgeni Rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara akiongea katika mahafali hayo.
Meneja Mkuu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, akiongea katika mahafali hayo
Mmoja wa wahitimu , Selina Mkaro kutoka kampuni  ya Kemanyaki Contractors akiongea kwa niaba ya wahitimu wenzake.
Mhamasishaji  (Motivational Speaker), Joel Nanauka,akiongea na wahitimu wa mafunzo hayo
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo wakipokea vyeti kutoka kwa Mgeni rasmi
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo wakipokea vyeti kutoka kwa Mgeni rasmi
Picha ya pamoja na wahitimu wakiwa na Mkuu wa wilaya ya Rorya na Meneja Mkuu wa Barrick North Mara
 
**

 

Programu ya maendeleo ya kibiashara ya Barrick, (Local Business Development Programme),  inayolenga kuimarisha uwezo wa biashara za ndani ili ziweze kunufaika na fursa zilizopo kwenye sekta ya madini imewafikia walimiki 19 wa kampuni za wafanyabiashara  mkoani Mara kupitia mafunzo maalum ya biashara ya siku mbili yaliyofanyika katika mgodi wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime ambayo yalifungwa na  Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rorya, Juma Chikoka, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, Said Mohamed Mtanda.

Wamiliki wa kampuni hizo ni wafanyabishara wanaotoka maeneo yaliyo jirani na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Akiongea wakati wa mahafali ya kumaliza mafunzo hayo,Meneja Mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, alisema mafunzo haya ni mwendelezo wa mkakati wa kampuni ya Barrick wa kuhakikisha wafanyabiashara wazawa wananufaika na fursa zilizopo katika migodi yake “Kuhitimu kwa kampuni hizi ni alama muhimu katika kukuza biashara ya wazawa katika mkoa wetu wa Mara,”alisema .

Lyambiko, alisema Kampuni ya Barrick Gold imeendelea kuwapa wazabuni wazawa fursa ya kuhudumia na kusambaza bidhaa katika mgodi huo ili kuunga mkoni juhudi zinazofanywa  na Serikali.

Alitolea mfano wa dola za Marekani milioni 37.4 sawa na takriban shilingi bilioni 95 ambazo zimelipwa na mgodi huo kwa wazabuni wazawa kwa mwaka 2023 huku ukitilia maanani falsafa ya ‘Local Content’.

Meneja Mkuu huyo alisema hadi sasa Mgodi wa Barrick North Mara, umesajili kampuni 118 ambazo zinapata fursa mbalimbali za kibiashara katika mgodi huo na zimetoa ajira kwa watu 1,144, wengi wao wakitokea  maeneo yanayozunguka mgodi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

“Jitihada hizi sio tu zimechangia kweye ustawi wa maendeleo ya jamii bali zimesaidia katika kuimarisha mahusiano yetu na jamii inayotuzunguka,” alisema ,Lyambiko.

 Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara katika mahafali hayo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rorya, Juma Chikoka, aliipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuanzisha programu ya kuwajengea wafanyabiashara uwezo na kuongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanawaongezea washiriki uelewa na yatawawezesha kuwa na vigezo vya kunufaika na fursa mbalimbali za kibiashara ndani na nje ya mgodi wa Barrick North Mara

 “Kama Serikali tunatambua mchango wa Barrick North Mara, na hii inatusaidia pia kufikia maendeleo ya kitaifa,” alisema Chikoka ambaye pia kwa sasa ni kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tarime.

Mwakilishi kutoka Tume ya Madini, Annasia Kwayu ambaye ni Meneja Ukaguzi wa Fedha, Kodi na Ushirikishwaji wa Watanzania  aliupongeza mgodi huo kwa kufanikisha mafunzo hayo ambayo yameendeshwa na Kampuni ya Impacten na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia huduma bora katika migodi nchini na aliwataka wahitimu wa mafunzo hayo kuzingatia waliyojifunza ili wakidhi vigezo vya kufanya biashara ndani nan je ya mgodi sambamba na kuimarisha biashara zao.

Kwayu, alisema mpango huo ni kielelezo halisi cha utekelezaji wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018 na marekebisho yake.

Mhamasishaji maarufu (motivational speaker) nchini, Joel Nanauka, alipata fursa ya kuzungumza na wahitumu hao kwa dakika kadhaa na kuwataka kuwa na maono ziadi huku wakijiepusha na watu wasiokuwa na maono.

Akiongea kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo hayo ambayo yamechukua miezi sita, Selina Mkaro kutoka kampuni  ya Kemanyaki Contractors,alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa wa kufanya biashara kwa ufanisi sambamba na kuwa na vigenzo vya kufanya biashara na Mgodi wa North Mara na sehemu nyinginezo.

About the author

mzalendoeditor