Kitaifa

UWIANO WA TIJA NA MASLAHI CHANZO CHA MATOKEO BORA YA KIUTENDAJI – NDEJEMBI

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya elimu Deogratius Ndejembi amesema ili kuwepo na matokeo bora ya kiutendaji kazi katika kutoa huduma bora kwa wananchi lazima tija na maslahi viwe na uwiano.

Naibu Waziri Ndejembi ameyasema hayo leo Machi 12,2024 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI cha kupitisha bajeti na mpango kazi kwa mwaka 2024/25.

“Hivyo ieleweke kuwa utendaji bora wa kazi na wenye tija kwa kuzingatia weledi na uwajibikaji utaiwezesha Serikali kuongeza mapato na hivyo kuwezesha kuongeza vile vile utoaji wa maslahi bora,”amesema.

Amesema kuwa madhumuni ya baraza la wafanyakazi ni kutoa fursa kwa watumishi kupitia kwa wawakilishi wao kujadiliana juu ya masuala mbalimbali ya msingi yanayohusu tija na ufanisi kwa upande mmoja na maslahi yao kama watumishi kwa upande mwingine.

“Baraza la wafanyakazi linaongeza ushiriki wa wafanyakazi katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za taasisi kama ilivyo fafanuliwa katika sheria ya majadiliano ya pamoja katika utumishi wa umma sura namba 105,”amesema.

Aidha amewasisitiza kuwa mikutano ya mabaraza ya wafanyakazi itumike katika kujadili malengo na mipango ya taasisi ikiwa ni pamoja na maslahi ya watumishi na kuongeza kuwa mabaraza hayo yanatakiwa kujadili utendaji kazi wa kila siku na jinsi ya kuboresha utendaji kazi zaidi.

“Hapa nisisitize sana kuna umuhimu wa kila mtumishi katika kila taasisi kufahamu malengo ya taasisi ( Vision and Mission) ili tuweze kwenda pamoja na tusihiahi kama headless chicken kuku ukimkata kichwa anaruka ruka hujui Mission na Vision inakwenda wapi kwahiyo ni muhimu sana kujadili hayo katika mabaraza haya,”amesisitiza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi na Naibu Katibu mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde amesema baraza la wafanyakazi liliundwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2003 kama yanavyoundwa mabaraza mengine katika uwajibikaji na ndiyo linalounganisha kati ya wafanyakazi na wakuu wa idara wengine na kuwafanya kutimiza wajibu wao katika utendaji wa kazi.

Amesema moja kati ya ajenda zitakazojadiliwa katika kikao cha baraza hilo ni kuhusiana na bajeti itakayoenda kusomwa bungeni mwezi ujao pamoja na kupanga mpango kazi utakao wasaidia kufikia malengo yao.

 

About the author

mzalendo