Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wanakutana kwenye kikao cha dharura kujadili machafuko yanayoendelea kushuhudiwa nchini Haiti, wakati huo magenge yenye silaha yakimshinikiza Waziri Mkuu Ariel Henry kujiuzulu.
Mkutano huu unakuja wakati kiongozi wa magenge hayo Jimmy Cherizier maarufu kwa jina la Barbecue, yanayodhibiti maeneo mengi ya jiji kuu Port-au-Prince, akionya kuwa hali itaendelea kuwa mbaya iwapo Ariel hataachia madaraka.
Barbecue, anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuacha kumuunga mkono Ariel, na kumshinikiza kujiuzulu la sivyo Haiti itashuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kuanzia wiki iliyopita wakati Waziri Mkuu huyo akiwa ziarani nchini Kenya, watu wenye silaha walianza kushambulia maeneo ya kimkakati kama uwanja wa ndege, magereza na vituo vya polisi.
Machafuko yanayoendelea yamesababisha kiongozi huyo wa Haiti kushinda kurejea nyumbani ripoti zikisema kuwa, kwa sasa yupo nchini Puerto Rico.
Haiti imeendelea kukumbwa na utovu wa usalama tangu mwaka 2021, alipouawa rais Jovenel Moise, na tangu kipindi hicho watu zaidi ya Elfu 15 wameyakimbia makaazi yao, huku idadi kubwa ya watu ambayo haijafahamika wakiripotiwa kuuawa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.