Featured Kitaifa

ZUNGUMZIENI MAFANIKIO YA SERIKALI-MSEMAJI MKUU WA SERIKALI 

Written by mzalendo

Na.Mwandishi Wetu-Arusha

Maofisa Habari na Mawasiliano wa Serikali nchini wametakiwa kuzungumzia mafanikio makubwa yaliyofanywa na Serikali katika sekta zote nchini.

Hayo yamesemwa leo na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo Bw. Mobhare Matinyi wakati akiongea na maafisa habari na mawasiliano wa Serikali kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Maafisa Habari wa Serikali (TAGCO) katika kituo cha Mkutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha.

Bw. Matinyi amesema kazi kubwa imefanyika hapa nchini katika sekta na maeneo mbalimbali, hivyo anatarajia maafisa habari hao kuzungumzia kila sekta bila kujali amebobea eneo gani.

“Fani hii ni pana sana,natarajia kila afisa habari na mawasiliano aweze kuzungumzia kila sekta au eneo katika uchumi, jiografia, mazingira na maeneo mengineyo hata kama umebobea eneo jingine au umehamia eneo jipya”.

Aidha, Bw. Matinyi amesema kwamba maafisa habari hao wanao wajibu wa kutekeleza yale yanayofanywa na Taasisi zao kwa kupata mrejesho toka kwa wananchi pamoja na kuhakikisha wanasaidia kukuza taswira nzuri za taasisi hizo.

Kwa upande mwingine Msemaji Mkuu huyo amewakumbusha maofisa habari hao kuhakikisha wanatuma ripoti zao za kila mwezi Idara ya habari-Maelezo ambao wana jukumu la kusimamia na kuratibu shughuli za kiserikali.

Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Maafisa Habari Serikalini (TAGCO) unafanyika jijini Arusha na unatarajia kumalizika leo na inawakutanisha maafisa habari na mawasiliano wa Serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

About the author

mzalendo