Featured Kimataifa

DKT. BITEKO: UCHORONGAJI VISIMA VYA JOTOARDHI KUANZA APRILI 2024

Written by mzalendo
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza baada ya kuwasili katika eneo lenye chanzo cha nishati ya Jotoardhi katika Mji wa Naivasha, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya.

Mbili
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko pamoja na viongozi wengine kutoka Tanzania wakikagua mitambo ya Jotoardhi iliyopo katika Mji wa Naivasha, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya (haipo pichani).
Tatu
Mitambo ya umeme wa Jotoardhi iliyo katika Mji wa Naivasha katika Kaunti ya Nakuru nchini Kenya.

…………………… 

*Lengo ni kuwa na vyanzo mchanganyiko vya umeme

*Kampuni ya KenGen ya Kenya na TGDC kushirikiana katika uhakiki

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema
kuwa kazi ya uchorongaji wa visima vya Jotoardhi nchini Tanzania
itaanza mwezi Aprili mwaka huu ili kuweza kuhakiki rasilimali ya
Jotoardhi iliyopo kabla ya kuanza kwa shughuli za uzalishaji umeme
kutokana na nishati hiyo.

 Dkt. Biteko amesema hayo baada ya kutembelea vyanzo na mitambo ya
kuzalisha umeme wa Jotoardhi katika Mji wa Naivasha, Kaunti ya Nakuru
nchini Kenya.

“Tumekuja kwenye mitambo ya kuzalisha umeme unaotokana na Jotoardhi
inayomilikiwa na kampuni ya uzalishaji umeme ya Kenya (KenGen) na
tumejionea jinsi walivyopiga hatua kwenye uendelezaji wa rasilimali
hii kwani tayari wanazalisha umeme wa Jotoardhi wa kiasi cha megawati
zaidi ya 799.” Amesema Dkt. Biteko

Amesema Tanzania kwa upande wake, tayari imeshatenga fedha kwa ajili
ya kuendeleza vyanzo vya Jotoardhi na kwamba kampuni ya KenGen mwezi
Aprili mwaka huu itakuwa mkoani Mbeya kwa ajili ya kuanza uchorongaji
vyanzo vya Jotoardhi katika eneo la Ngozi na Kiejo-Mbaka kwa
kushirikiana na kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).

Dkt. Biteko ameipongeza kampuni ya KenGen ya Kenya kwa hatua kubwa
waliyofikia katika uendelezaji wa Jotoardhi  ambapo zaidi ya asilimia
60 ya umeme nchini humo unatokana na nishati hiyo.

Ametanabaisha kuwa, Tanzania  imeamua kuongeza vyanzo vya uzalishaji
umeme na sasa nguvu kubwa inawekwa kwenye kuendeleza miradi kama hiyo
ya Jotoardhi ili kupata umeme wa kutosha kwa ajii ya wananchi.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Maendeleo ya Jotoardhi katika kampuni
ya KenGen, Peketsa Mangi amesema kuwa, nchi hiyo imekuwa na
ushirikiano mzuri na Tanzania katika kuhakikisha nchi hizo
zinafanikiwa katika uendelezaji wa Jotoardhi.

Ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuipatia nafasi KenGen kufanya
kazi kwa pamoja na wataalan kutoka TGDC ili kuchimba visima vya
uhakiki wa rasilimali hiyo nchini na kueleza kuwa, kampuni hiyo ipo
tayari kufanya kazi husika kwa mafanikio.

Viongozi walioambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
kwenye ziara hiyo ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Balozi wa Tanzania nchini Kenya,
Mhe. Benard Kibesse na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.

About the author

mzalendo