Featured Kitaifa

KWARESMA ITUMIKE KWA MATENDO YA HURUMA-PADRI MASANJA

Written by mzalendo

Adeladius Makwega-MWANZA

Wakristo wameambiwa kuwa Jumatano ya Majivu , wanapakwa majivu hayo kama ishara ya toba na katika kipindi hichi wanatakiwa kusafiri katika unyofu wa moyoni.

Hayo yamesemwa katika Kanisa la Bikira Maria Malkia wa Wamisionari , Parokia ya Malya , Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Padri Samson Masanja katika misa ya Jumatano ya Majivu iliyoanza saa 9 alasiri na kumaliza saa 11 jioni ya Jumatano ya Februari 14, 2024.

Padri Masanja aliongeza kuwa

“Kila Mkristo anatakiwa kujiweka mikononi mwa Mungu, kukumbuka sana kusoma neno la Mungu na pia kuyafanya matendo ya huruma kwa wahitaji.”

Akihitimisha misa hiyo, Padri Masanja alikumbusha waamini hao kukumbuka kuwa Jumapili ijayo ya Februari 18, 2024 kila Kigango cha Parokia ya Malya kutakuwa na zoezi na uwezeshaji (Kuwategemeza ) makatekista maana wao ni walimu wanaotoa mafundisho ya kiroho katika kila kigango, hivyo waamini wote aliomba wajiandae

Wakati misa hiyo inafanyika, hali ya hewa ya Malya ilikuwa na ngurumo za hapa na pale, manyunyu kidogo na joto kali, huku kanisa hilo likijaa waamini wengi ambapo umati mkubwa ulijaza ndani ya kanisa, nalo kundi kubwa la pili la waamini likiujaza pia uwanja kando ya kanisa hili .

Kutokana na umati huo mkubwa, zoezi la kupakwa majibu liliendelea na makatekista wawili mara baada ya misa kumalizika, nia ni kutoa nafasi kwa waamini ambao walichelewa kupakwa majivu awali.

Mandhari ya kiwanja cha kanisa hilo ilipambwa na misururu mirefu ya waamini wa rika zote, wakijongea katika lango la kanisa hilo na makatekista hao wawili mama na baba walisimama katika ngazi za lango kuu la kanisa na kuwapaka majivu.

Wakati misa hiyo inaanza hadi inamalizikia pembezoni mwa kanisa hili ilisikika sauti ya jenereta ikiunguruma ambapo ilitumika kufua umeme uliotumika kutoa mwanga kanisa hapo maana kwa mchana mzima ya Februari 14, 2024 eneo lote la Malya halikuwa na umeme kwani ulikatika asubuhi na kurudi saa 12, 00 jioni.

About the author

mzalendo