Featured Kimataifa

TANZANIA YAPITISHA KUWA MWENYEJI WA KONGAMANO LA PETROLI LA AFRIKA MASHARIKI

Written by mzalendo

 

Mwenyekiti wa Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Shaibu Hassan Kaduara ambaye ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar (kulia) akizungumza katika Mkutano wa Baraza hilo ulioanza tarehe 12 Februari 2024 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini na kuhitimishwa tarehe
14 Februari 2024.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, akizungumza katika Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulioanza tarehe 12 Februari 2024 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha na kuhitimishwa tarehe 14 Februari 2024.

Mwenyekiti wa Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Shaibu Hassan Kaduara ambaye ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar (wa Pili kushoto, mbele) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Jumuiya ya EAC waliohudhuria Mkutano wa Baraza hilo ulioanza
tarehe 12 Februari 2024 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha na kuhitimishwa tarehe 14 Februari 2024.

……………..

 Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulioanza tarehe 12 Februari 2024 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha umehitimishwa tarehe 14 Februari 2024.

Katika mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Shaibu Hassan Kaduara ambaye ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar ulipendekeza kuwepo kwa mkakati wa pamoja wa Jumuiya wa kukabiliana na kuzuia uharibifu wa miundombinu mbalimbali ya nishati ikiwemo ya usambazaji na usafirishaji.

Aidha, Mkutano huo ulitoa mapendekezo kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuongeza kasi na bajeti ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati katika ngazi ya Taifa na Jumuiya itakayoimarisha upatikanaji wa nishati ya kutosha, bei nafuu, endelevu na salama kwa maendeleo ya Jumuiya na watu wake.

Akifungua mkutano huo Waziri Kaduara alieleza kuwa, Jumuiya itaweza kuchochea ongezo la uwekezaji, ajira na ukuaji maradufu wa uchumi na biashara endapo pamoja na masuala mengine kutakuwepo na upatikanaji wa nishati ya uhakika na salama.

“Sekta ya Nishati ina umuhimu wa kipekee katika kufanikisha  maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Jumuiya, hivyo umuhimu wa  upatikanaji wa nishati ya uhakika, salama na gharama nafuu ni jambo la lazima na sio hiyari kwani ni kichocheo cha kuvutia uwekezaji na kufanya bidhaa na huduma zinazozalishwa kuwa shindani katika soko la ndani na
kimataifa”.  Alieleza Waziri Kaduara

Vilevile, Mhe. Kaduara alitumia fursa ya mkutano huo kutoa mwaliko kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kushiriki katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaofanyika tarehe 25 Februari 2024.

Mkutano huo wa Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu ambao ulipitia na kujadili utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya. Pia ulipokea na kujadili taarifa za
maendeleo ya sekta ya nishati katika maeneo ya umeme, mafuta, gesi na nishati jadidifu.

Mwenyekiti wa Mkutano huo wa Makatibu Wakuu ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara inayohusika na masuala ya Afrika Mashariki katika Jamhuri ya Kenya, Abdi Dubati alieleza kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa jitihada za Wakuu wa Nchi wanachana wa Jumuiya za kuhahikisha sekta ya nishati inaimarika ili kuchagiza maendeleo ya Jumuiya kutokana na mchango wake mkubwa katika kuvutia wawekezaji, kukuza biashara na uzalisha wa bidhaa viwandani.

Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo Mhandisi Felchesmi  Mramba ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati alieleza kuwa, kikao hicho kinatoa fursa ya kuunganisha nguvu na kuweka mikakati ya pamoja katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati ikiwemo umeme.

Katika Mkutano wa ngazi ya Watalaam kulijadiliwa taarifa mbalimbali za maendeleo ya sekta ya nishati katika Jumuiya. Vilevile kuweka mikakati ya pamoja ya kutatua chagamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika na endelevu katika Jumuiya.

Akizungumza  kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa ngazi ya wataalam Mwenyekiti wa Mkutano huo, Petro Lyatuu, Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Nishati – Tanzania alieleza kuwa, licha ya mafanikio yaliyofikiwa katika sekta hiyo bado mchango na weledi wa wataalam hao unahitajika ili kutatua changamoto zilizopo na hatimaye kufikia malengo yanayotarajiwa na Jumuiya.

Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo uliipitisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kongamano na Maonesho ya 11 ya Petroli Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika tarehe 7 hadi 9 Machi 2025.

Kongamano hilo litakalohusisha wadau kutoka serikalini na sekta binafsi linalenga kubadilishana taarifa kuhusu hali ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya, na kutangaza fursa zilizopo katika ukanda kwenye sekta hiyo, hususan fursa za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.

About the author

mzalendo