Featured Kitaifa

SERIKALI KUENDELEA NA UCHIMBAJI WA VISIMA VYA MAJI NACHINGWEA

Written by mzalendoeditor

 

KATIKA kuboresha huduma ya maji kwenye Kata za Matekwe, Kiegei na Namapwia, zilizopo Nachingwea Mkoani Lindi
Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 inaendelea na zoezi la uchimbaji wa visima 4 ambapo kisima kimoja tayari kimechimbwa katika Kijiji cha Kilimarondo na uchimbaji wa visima vitatu unaendelea na unatarajiwa kukamilika Mwezi Juni, 2024.

Hayo yamesemwa leo Februari 14 2024 na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) wakati akijibu swali la mbunge wa Viti maalum Tecla Mohamed Ungele ambae aliuliza ni lini wananchi wa Kata za Nachingwea, Kiegei, Matekwe na Namapwia- Nachingwea Lihimalya na Kandawale- Kilwa watapatiwa maji.

Mahundi amesema kwenye Kata ya Nachingwea, Serikali inaendelea na kazi ya usanifu wa mradi pacha toka vyanzo vya Mbwinji na unatarajia kukamilika mwezi Juni, 2024, ambapo utekelezaji wa mradi utaanza katika Mwaka wa Fedha 2024/25.

“Kwa upande wa Kata ya Kandawale yenye jumla ya Vijiji Vinne (4), Vijiji viwili (2) vya Kandawale na Mtumbei vinapata huduma ya majisafi na salama kupitia miradi iliyojengwa yenye jumla ya vituo 13,

“Vijiji vya Ngarambi na Matewa vinatarajiwa kuchimbiwa visima katika Mwaka wa Fedha 2024/25. Kwa upande wa Kata ya Lihimalya, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2024/25 itafanya upanuzi wa mradi wa maji wa Pande kwa ajili ya kufikisha huduma ya maji kwenye Vijiji vya kata hiyo” amesema Mhandisi Mahundi

About the author

mzalendoeditor