Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, imesema kuwa nchi hiyo itatuma wanajeshi 2,900, kama sehemu ya mchango wake kwa kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kinachotarajiwa kukabiliana na makundi yenye silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
Operesheni hiyo ya mwaka mmoja ni ya kati ya Desemba 15, mwaka 2023 na Desemba 15, mwaka huu, na itagharimu takriban dola za Marekani milioni 105.75.
SADC, yenye nchi wanachama 16, iliidhinisha vikosi kutumwa mashariki mwa Kongo mwezi Mei mwaka jana, kusaidia nchi hiyo, msambazaji mkuu wa cobalt duniani na mzalishaji mkuu wa shaba barani Afrika, kukabiliana na hali ya kukosekana kwa utulivu na kuzorota kwa usalama katika eneo la mashariki.
Miongo kadhaa ya migogoro mashariki mwa DRC, kati ya makundi hasimu yenye silaha, yakizozania ardhi na rasilimali, imepelekea vifo vya mamia ya maelfu ya watu na kusababisha zaidi ya watu milioni 7 kufurushwa makwao.
Kikosi cha SADC kinajumuisha wanajeshi kutoka Malawi, Afrika Kusini na Tanzania. Kutumwa huko kunajiri wakati Kongo inapambana na waasi wa M23 wanaoongozwa na Watutsi, ambao mashambulizi yao katika siku za hivi karibuni, yanatishia mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma.