Uncategorized

MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII INAONDOA UTEGEMEZI UZEENI

Written by mzalendo

 

Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Janeth Hiza, akitoa mada kuhusu elimu ya fedha kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa faida ya wazee na wastaafu, wakati wa mafunzo ya huduma za fedha kwa wasanii kutoka Shirika la TACCI mkoani Morogoro, watakao husika kutoa elimu ya fedha vijijini.

Mkurugenzi wa Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia TACCI, Bi. Aline Augustin na Mtaalamu wa Sanaa za Jukwaani, Bw. Harrison Kisaka, wakisikiliza mada ya uwekaji akiba, wakati wa mafunzo ya huduma za fedha kwa wasanii kutoka Shirika la TACCI mkoani Morogoro, ambao wanalengwa kutoa elimu ya fedha vijijini.

Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro,akielezea kuhusu umuhimu wa kuweka akiba akiba yenye malengo kwa Wasanii kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI), mkoani Morogoro.

Msanii kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji Elimu ya Uraia, Bw. Rajabu Athuman Zegegia ambae ni mcheza ngoma, akiuliza jambo wakati wa mafunzo ya huduma za fedha kwa wasanii kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji Elimu ya Uraia – TACCI, mkoani Morogoro, ambao wanalengwa kutoa elimu ya fedha vijijini.

Msanii kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia, Bw. Iddy Athumani, ambae ni muingizaji, akieleza changamoto wanazoziona kwa watoa mikopo wasio sajiliwa wakati wa mafunzo ya huduma za fedha kwa wasanii kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji Elimu ya Uraia -TACCI, mkoani Morogoro, ambao wanalengwa kutoa elimu ya fedha vijijini.

Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro (wa saba kulia) na Mkurugenzi wa Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia TACCI, Bi. Aline Augustin (wa sita kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa kutoka Wizara ya Fedha na Wasanii kutoka TACCI, baada ya mafunzo ya elimu ya fedha mkoani Morogoro, yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kupeleka elimu hiyo maeneo ya vijijini.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Morogoro)

Na. Peter Haule, WF, Morogoro

Wananchi wanatakiwa kupata elimu ya fedha na kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuwasaidia wanapozeeka au kustaafu kazi ili kuondoa utegemezi.

Wito huo umetolewa mkoani Morogoro na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Janeth Hiza, wakati wa Mafunzo ya Elimu ya Fedha kwa Wasanii kutoka Shirika la Kijamii linalojishughulisha na utoaji wa Elimu ya Uraia (TACCI) wanaolengwa kupeleka elimu ya fedha vijijini.

Alisema kuwa Serikali imeweka Sera, Sheria, Kanuni na miongozo ambayo inamtaka kila mwajiri awe sekta ya umma au binafsi kuwaandalia wafanyakazi wake utaratibu wa kupata mafao baada ya kustaafu kwa ugonjwa, kufukuzwa kazi au kustaafu kwa kigezo cha umri.

“Kwa binadamu aliye kamilika anahitaji fedha na matumizi, kama ukiwa na fedha nyingi wakati wa ujana kuna wakati utafika nguvu zitaisha jambo litakalokufanya uhitaji Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ukusaidie ili uishi maisha yenye staha uzeeni, hapo ndipo linapokuja suala la umuhimu kujiunga kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii”, alieleza Bi. Hiza.

Akitoa mada katika Mafunzo kwa Wasanii wa TACCI, Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, alisema kuwa elimu ya fedha inamsaidia kila mtu kupanga maisha kwa ufasaha kwa kufahamu umuhimu wa usimamizi wa fedha binafsi, kutambua umuhimu wa kuweka akiba na eneo sahihi la kukopa

Vilevile alisema kuwa elimu ya fedha inasaidia mtu kuelewa umuhimu wa kulipa madeni anapokopa pamoja na kuzifahamu na kuzichangamkia fursa nyingine zinazopatikana katika sekta ya fedha zikiwemo uwekezaji katika mitaji ya dhamana.

“Katika ngazi ya mtu binafsi usipokuwa na elimu sahihi katika utekelezaji wa jambo lolote ni rahisi kushindwa kufikia malengo na kuwatupia lawama watu wengine ambao hawahusiki na kushindwa kwako”, alisema Bw. Kimaro.

Bw. Kimaro alisema program ya elimu kupitia Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha inayotolewa na Wizara ya fedha inasaidia kujua ni kundi lipi na idadi gani na wapi elimu inatakiwa kutolewa ili kutoa uelewa wa kutosha kwa wananchi, kuwawezesha kuingia katika kadhia ya hasara inayotokana na uelewa mdogo wa masuala ya fedha.

Alieleza kuwa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha unalengo la kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2025, asilimia 80 ya wananchi wawe na uelewa wa kutosha wa elimu ya fedha.

Alibainisha kuwa Walengwa wa program ya elimu ya fedha ni watumishi wa umma, wanafunzi, wakufunzi, wanawake, vijana, watu wenye mahitaji maalum, wajasiliamali wadogo na wa kati, asasi za kiraia, wahariri na waandishi wa vyombo vya habari, watoa huduma za fedha, Watoto na umma kwa ujumla.

“Maendeleo ya Sekta ya Fedha yatasaidia upatikanaji na ugawaji wa rasilimali fedha kwa ukuaji wa uchumi na kuondoa umasikini, fani pekee ambayo kila mtu anapaswa kuwa nayo ni elimu ya fedha kwa kuwa kila kazi inayofanywa ina sehemu ya kutafuta fedha,”, alisisitiza Bw. Kimaro

Kuhusu Sekta ndogo za fedha, Bw. Kimaro alisema zinajumuisha, Benki, Bima, Hifadhi ya Jamii, Masoko ya Mitaji na Dhamana na watoa huduma ndogo za Fedha (Micro Finance)

Kwa upande wake Mtaalamu wa masuala ya fedha wa Wizara ya Fedha, Bi. Grace Muiyanza alisema kuwa Watoa huduma za fedha wapo katika madaraja manne, Daraja la kwanza linahusika na Benki na daraja la pili ni wale ambao hawapokei amana (wakopeshaji binafsi na kampuni) ambapo madaraja hayo yanasimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)

Alieleza kuwa Daraja la tatu ni wale wanapokea amana ambao wanasimamiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika na daraja la nne ni vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha (CMG), ambavyo vinasimamiwa na TAMISEMI, mamlaka ambayo wamekasimishwa na Benki Kuu ya Tanzania-BoT

Bi. Muiyanza alieleza kuwa vikundi vya kijamii vya watoa huduma ndogo za fedha ambavyo vipo daraja la nne vinatakiwa kuhusisha wanakikundi kuanzia 10 hadi 50 wenye malengo ya aina moja.

Aliongeza kuwa baada ya uongozi wa kikundi kuridhia kusajili kikundi, wanatakiwa kuandaa taarifa za msingi kupitia portal na kuwasilisha Mamlaka za Serikali za mitaa, Halmashauri, Manispaa au Jiji kwa ajili ya mapitio ya awali na kama taarifa zao zitakuwa sahihi zitarudishwa kwenye kikundi zikiwa na cheti cha usajili wa kikundi.

Bi Muiyanza alisema kuwa Taarifa za msingi zinazotakiwa ni pamoja na muhtasari wa kikao cha uanzilishi, orodha ya wanakikundi walioonesha nia ikiwa ni pamoja na michango ya awali waliyoitoa, barua ya utambulisho ya kata au Kijiji, katiba ya kikundi iliyoridhiwa kuitumia na wanakikundi wote.

Alifafanua kuwa Katika zoezi la kuwezesha usajili wa kikundi, wanakikundi wenyewe wanaweza kuingia kwenye tovuti na kufanya usajili au wakamhusisha Afisa maendeleo ya jamii aliyepo kwenye Mamlaka ya Serikali ya Mtaa au wakamtumia mhamasishaji wa biashara za huduma ndogo za fedha.

Aidha Bi. Muiyanza alisema kuwa Mhamasishaji anatakiwa kuwa mtu mwenye weledi kwenye masuala ya fedha lakini awe amesajiliwa katika Mamlaka ya Serikali ya Mtaa na amepata elimu ya masuala ya fedha, usimamizi na uendeshaji wa vikundi.

About the author

mzalendo