Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amewataka Wanataaluma kutafiti na kujadili historia ya nchi kwa uwazi na uzalendo ili kuhakikisha haipotoshwi hivyo kusaidia vizazi vijavyo kuwa na taarifa sahihi ajili ya maendeleo.
Prof. Mkenda ametoa rai hiyo Januari 06, 2024 Visiwani Zanzibar wakati akifungua Kongamano la Kitaaluma la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), ambapo amesema Wanataaluma wanapaswa kushiriki katika kuenzi Mapinduzi hayo ili kujenga jamii yenye ustawi wa kisiasa na hata kiuchumi.
“Vyuo Vikuu vina jukumu la kuchambua historia ya nchi yetu kwa uwazi na uzalendo ili kuhakikisha inatunzwa na kwamba haipotoshwi ili vizazi vinavyokuja vielewe mazuri yaliyofanyika na jinsi yalichochea uchumi ambayo ni tafsiri sahihi ya kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu inayosema _Tuimarishe Uchumi, Uzalendo Amani na Umoja kwa Maendeleo ya Taifa letu_” alisema Prof. Mkenda.
Aidha amesisiza jamii kuzingatia na kuikumbuka kikamilifu dhana kubwa ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964, inayosisitiza binadamu wote ni sawa na kwamba inapaswa kutopuuziwa katika kuhakikisha inaendeleza ustawi kwa watu wote bila kujali hali zao.
“Zanzibar ni sehemu ya Muungano wa Tanzania, leo hii ndani ya nchi yetu tunajivunia tunaye Rais Mwanamke, tunampongeza sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuenzi tunu zetu na kutuletea Maendeleo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo Uchumi, Elimu, Afya na miundombinu mingine” alibainisha Waziri Mkenda.
Pia Waziri Mkenda amewataka Washiriki wa Kongamano hilo kutumia fursa hiyo kujadili na kutafsiri kwa vitendo matunda ya Mapinduzi kwa mnasaba wa kuwaletea wananchi Maendeleo makubwa zaidi pamoja na kushiriki katika maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.
Nae Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Prof. Mohamed Makame ameeleza kuwa Chuo hicho tangu kianze Mwaka 2001 kinaendelea kuthamini , kuheshimu na kuenzi mambo yote yaliyoanzishwa na kuasisiwa na kwamba inajivunia Maadhimisho ya Mapinduzi hayo ambayo yameleta mafanikio makubwa ikiwepo kuwezesha kuwa na Uhuru, Umoja na mshikamano wa dhati.
Ameongeza kuwa SUZA inaendelea na harakati za kuleta mageuzi kwa kutekeleza majukumu makuu manne ikiwa ni pamoja na kutoa Taaluma kuanzia ngazi ya Stashahada hadi shahada ya Uzamivu, kufanya tafiti mbalimbali zinazotoa matokeo kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi pamoja na kutoa ushauri wa kitaaluma kwa Wadau mbalimbali hasa kwenye sekta ya biashara.
Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Mhe. Ayoub Mohamed amekishukuru Chuo cha SUZA kuandaa Kongamano hilo muhimu, akisema limekuja muda muafaka kwani limetoa nafasi ya watu kujadiliana juu masuala mbalimbali ya maendeleo.
“Kongamano hili litasaidia kutoa uelewa kwa vijana hasa Wanafunzi, lakini na wananchi kwa ujumla juu ya historia ya Zanzibar tangu ipate uhuru, ambapo leo tumeangazia dhamira ya Mapinduzi na malengo ya muasisi Mhe. Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na mahali tulipo” Alieleza Kiongozi huyo.
Aidha amesema kupitia Kongamano hili pia wamepata nafasi ya kuangazia hali ya ukuaji wa sekta ya elimu kabla, wakati na baada ya Mapinduzi, pamoja na kutathimini hali ya kuimarika kwa Uchumi katika kipindi cha miaka 60.