Kitaifa

WANAFUNZI WANAOMUDU LUGHA YA KIINGEREZA WAONGEZEKA-MCHENGERWA

Written by mzalendo

OR-TAMISEMI

Viashiria vya upimaji wa utendaji kazi wa walimu kuanzia Januari hadi Desemba 2023 vimeonyesha kuna ongezeko la wanafunzi wa darasa la kwanza wanaomudu stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kutoka asilimia 35 hadi 94.4.

Akifunga leo kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi Elimu na Maafisa Elimu wa Halmashauri kilichofanyika Manispaa ya Morogoro, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema
idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaomudu stadi za nne za ligha ya Kiingereza (Kusikiliza, Kuongea, Kusoma na Kuandika) imeongezeka kutoka asilimia 32 hadi 82.

Aidha, amesema kwa Darasa la II umahiri wa Stadi za KKK umeongezeka kutoka asilimia 77.9 hadi 95 huku idadi ya wanafunzi wa darasa la tatu wenye uwezo wa kujitambulisha na kuelezea mazingira yao kwa lugha ya kiingereza umeongezeka kutoka asilimia 35 hadi kufikia asilimia 77 mwezi Desemba 2023;

Waziri Mchengerwa kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi waliomaliza Elimu ya Msingi Mwaka, 2023 kutoka asimilia 79.82 kwa mwaka 2022 hadi asilimia 80.58 mwaka 2023.

“Wanafunzi wa sekondari wanaopata chakula cha mchana shuleni wameongezeka kutoka asilimia 50.41 hadi kufikia asilimia 62.69 Desemba 2023. Na katika kipindi hicho, wanafunzi wa Shule za Msingi wanaopata chakula shuleni wameongeza kutoka asilimia 50 hadi kufikia asilimia 66.4.”

“Nitumie fursa hii wapongeza kwa dhati walimu wote wa shule za msingi na Sekondari nchini pamoja na wasimamizi wa elimu katika ngazi za Kata, Halmashauri, Mikoa na Taifa kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya katika kuhakikisha wanafunzi wanapata ujuzi, maarifa na stadi,”Mhe. Mchengerwa.

Amewapongeza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na viongozi wa kisiasa wote kwa jitihada zao na ushirikiano wanaowapa walimu katika kutekeleza majukumu yao.

About the author

mzalendo