Na. Asila Twaha, OR – TAMISEMI
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)Bw. Adolf Ndunguru amewataka Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha wanafuatilia miradi ya elimu na kuikamilisha ifikapo tarehe Januari 15, 2024.
Katibu Mkuu Ndunguru amesema hayo leo terehe 4 Januari, 2024 wakati akifungua kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi Elimu na Maafisa Elimu wa Halmashauri Kilichofanyika Manispaa ya Morogoro.
Amesema mwaka 2020/21 hadi 2023/24 Serikali imetoa fedha jumla ya shilingi trilioni 1.41 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za awali, msingi na sekondari. Aidha, amesema fedha hizo ziliwezesha kujenga shule mpya 380, vyumba vya madarasa 8,964, mabweni 48, matundu ya vyoo 25,688, nyumba za walimu 857, ujenzi wa mabwalo 6 na ukarabati wa shule na vituo vya walimu 396 kwa elimu ya awali na msingi.
Na kwa upande wa elimu ya sekondari amesema, zimejengwa shule mpya 460, vyumba vya madarasa 13,990, mabweni 1,135, maktaba 4, maabara 295 na mabwalo 103.
Amesema pamoja na jiitihada na dhamira njema ya Serikali katika kutekeleza miradi ya elimu lakini bado hajaridhishwa na baadhi ya watendaji ambao wanashindwa kusimamia na kukamilisha utekelezaji wa baadhi ya miradi kwa muda uliopangwa akitolea mfano kwa baadhi ya mikoa ambayo ujenzi wa miundombinu ya shule bado upo chini ya asilimia 50 licha ya maelelekezo ya Serikali yaliyoelekeza ujenzi ukamilike kabla ya terehe 30 Disemba, 2023.
“Viongozi wa Mikoa na Halmashauri ambazo ujenzi wa miundombinu ya shule haijakamilika mnatakiwa kujitafakari sana” amesisitiza Nduguru.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Nduguru amewataka maafisa hao kusimamia kikamilifu ufundishaji na ujifunzaji shuleni na kuhakikisha walimu wasiotimiza wajibu wao wanachukuliwa hatua stahiki, huku akiwataka kila Afisa elimu wa Mkoa na Halmashauri ahakikishe kuwa wanafunzi wote wa darasa la III na kidato cha kwanza wanamudu stadi za lugha ya kiingereza ifikapo mwisho wa mwaka2024, kuhakikisha wanashirikiana na wadau wengine kuwa wanafunzi wote wa darasa la I na darasa II wanamudu stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ifikapo mwisho wa mwaka.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -TAMISEMI anayeshughulikia elimu Dkt. Charles Msonde amewataka maafisa hao kutambua nafasi walizonazo kwa kufanya kazi kwa bidii na waledi na kushirikiana na kutoa wito wahakikishe wanawahudumia walimu kwa upendo, kuwasaidia, kuwasikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili na kuwatia moyo akisisitiza kwa kufanya hivyo itafanya kila mtu kufanya kazi zake kwa ufanisi na kutoa matokeo chanya ambayo ndiyo lengo la Serikali la kuwahudumia wananchi wake.