Featured Kitaifa

WAZIRI UMMY AKEMEA VIKWAZO VYA HUDUMA KWA WAJAWAZITO WASIOAMBATANA NA WENZA KLINIKI

Written by mzalendo

Na. WAF – Tanga

Waziri wa Afya Mhe. Ummy mwalimu ametaka kutowekewa vikwazo kwa mama mjamzito pindi anapoenda kliniki ya mama na mtoto bila ya kuwa na mwenza wake.

Waziri Ummy amesema hayo leo Novemba 30, 2023 kwenye Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.

“Tusiweke vikwazo kwa wanawake ambao wamepata ujauzito na wanaenda kliniki bila ya wenza wao kupata huduma, tuwashauri na tuwape elimu ili waende na wake zao lakini tusiwanyime huduma sababu hawakwenda na wenza wao.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, wanawake wengi wanapewa ujauzito na wanaachwa na wanaume wakihangaika peke yao l, utamlazimisha vipi aende na mwanaume wakati amemuacha.

Waziri Ummy amepiga marufuku kulazimisha mwanamke mjamzito kwenda na mwenza wake kliniki ili kupata huduma.

“Hii imepelekea wanawake wanatafuta bodaboda au mwanaume yeyote ampeleke kliniki ili apate huduma hii haikubaliki.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, inapaswa wanaume wahamasishwe, wapewe elimu kuwa hili ni muhimu baba na mama wote wakaenda kwa pamoja wakaenda kliniki lakini sio kuwalazimisha wanawake.

About the author

mzalendo