Featured Kitaifa

SERIKALI YAIPONGEZA MIGODI YA BARRICK NORTH MARA NA BULYANHULU KWA KUZALISHA AJIRA,KUWEZESHA VIJANA KIUCHUMI NA KUFANIKISHA MIRADI YA KIJAMII

Written by mzalendoeditor
Timu ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wakipata maelezo kuhusiana na mradi wa kilimo biashara ulioanzishwa na mgodi wa Barrick North Mara kwa ajili ya kuwawezesha vijana katika kijiji cha Nyangoto wilayani Tarime wakati walipofanya ziara ya kikazi mgodini hapo jana na kutembelea miradi ya kijamii inayotekelezwa na Mgodi.Wengine pichani ni baadhi ya vijana wanufaika wa mradi huo Meneja Mahusiano ya Jamii wa Barrick North Mara, Francis Uhadi (wa tatu kutoka kulia mwenye miwani) akitoa maelezo kwa timu ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu waliofanya ziara ya kikazi mgodini hapo jana na kutembelea miradi ya kijamii inayotekelezwa na Mgodi.

Timu ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wakiwa wamevaa vifaa husika kwa ajili ya kwenda kuona shughuli za uchimbaji madini chini ya ardhi (underground) eneo la Gokona, katika mgodi wa Barrick North Mara, wakati waliofanya ziara ya kikazi mgodini hapo jana na kutembelea miradi ya kijamii inayotekelezwa na Mgodi.
Timu ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wakiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa idara mbalimbali za Mgodi wa Barrick North Mara, wakati waliofanya ziara ya kikazi mgodini hapo na kutembelea miradi ya kijamii inayotekelezwa na Mgodi huo.
Timu ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (kushoto) wakipata maelezo ya utendaji wa shughuli za mgodi wa Barrick North Mara wakati walipofanya ziara ya kikazi mgodini hapo.
****
 
Timu ya Wakurugenzi watano kutoka vitengo mbalimbali vya Ofisi wa Waziri Mkuu, wamefanya ziara ya kikazi katika migodi ya Barrick North Mara na Bulyanhulu na wameeleza kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na migodi hiyohususani katika maeneo ya kutoa ajira kwa Watanzania, kuwezesha vijana kiuchumi na kufanikisha miradi ya kijamii.
 
Wakurugenzi hao wenye dhamana ya masuala ya kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu, waliyasema hayo wakati wa ziara yao ya siku 4 katika migodi hiyo inayoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
 
Akiongea kwa niaba ya Maofisa wenzake waliopo katika ziara hiyo,Mkurugenzi wa Ukuzaji Tija,Yohana Madadi,alitoa pongezi kwa migodi hiyo kwa kazi nzuri katika kuzalisha fursa za ajira sambamba na kufanikisha miradi mbalimbali ya kusaidia jamii zinazozunguka maeneo ya migodi hiyo.
 
Meneja Rasilimali Watu wa Barrick North Mara, Ivo Masanja, alieleza ujumbe huo kuwa hadi sasa mgodi wa Barrick North Mara umeajiri watu 1,391 ambapo asilimia 96 kati yao ni Watanzania na asilimia 67 wanatoka katika vijiji vinavyouzunguka maeneo ya mgodi huo.
 
“Hivyo idadi ya wageni ambao ni wataalamu (experts) walioajiriwa katika mgodi huo imepungua hadi asilimia nne. Aidha, mgodi huo unafanya kazi na wakandarasi 248 ambapo kati ya hao, asilimia 97.5 ni Watanzania”, alisema
 
Masanja, alisema mgodi huo una mpango wa kuongeza idadi ya wafanyakazi wanawake, sambamba na kuendelea kuwashawishi Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi kurudi nyumbani na kuwapatia ajira.
 
Kwa upande wake Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi aliwaeleza Wakurugenzi hao kutoka OWM kuwa mahusiano yao na jamii inayowazunguka yameendelea kuimarika, huku akitaja mradi wa kilimo biashara waliouanzisha kuwainua vijana kiuchumi kama ya moja ya mafanikio yanayoshuhudiwa.
 
“Tayari vijana wanaonufaika na mradi huu wa kilimo biashara wamepata mauzo ya shilingi milioi 164 na tunataka baadaye utumike kama shamba darasa,” alisema Uhadi.
 
Alisema asilimia 40 ya mbogamboga na viungo vinavyozalishwa katika mradi huo inauzwa katika mgodi wa Barrick North Mara kupitia Kampuni ya AKO, na asilimia 60 inauzwa kwenye masoko huria nje ya mgodi.
 
Kwa upande mwingine, Meneja huyo wa mahusiano alisema mgodi huo umeweka mfumo mzuri wa kupokea na kutatua malalamiko ya wananchi.
 
Hata hivyo, alitaja vitendo vya uvamizi (intrusions), uporaji wa mawe ya dhahabu, uharibifu wa miundombinu na uchimbaji wa madini usio halali kama matatizo makubwa yanayoukabili mgodi huo kwa sasa.
 
Katika tamko lao Wakurugenzi hao kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu waliahidi kushirikiana na migodi ya Barrick kutunisha mfuko wa kuwezesha vijana kiuchumi, ili waweze kukidhi mahitaji yao na kuchangia maendeleo ya taifa.
 
Walisema hatua hiyo itasaidia kupunguza vitendo vya uvamizi wa mogodi na kuanza kuchangamkia fursa nyingine za kuwawezesha kujiletea maendeleo.
 
“Mmefanya mambo makubwa sana kwenye jamii ikiwemo huu mpango wa kuwajengea vijana uwezo kujiajiri kupitia kilimo na ninyi kuwa sehemu ya soko la bidhaa wanazozalisha,” alisema Dkt Mwiga Mbesi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana.
 
Kwa mujibu wa Dkt Mwiga, kwa sasa vijana wana fursa ya kupata mkopo wa hadi shilingi milioni 50 katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ulio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
 
Katika ziara hiyo, timu hiyo ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu iliongozwa na Mkurugenzi wa Ukuzaji Tija, Yohana Madadi ambaye alieleza kuridhishwa na fursa za ajira, uwezeshaji vijana na miradi ya kijamii zilizotengenezwa na migodi hiyo.
 
Wakurugenzi wengine kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu walioshiriki ziara hiyo ni Amosi Nyandwi (Taarifa za Soko la Ajira), Joseph Nganga (Huduma za Ajira na Kissa Kilindu anayeshughulikia Ukuzaji Ajira.
 

About the author

mzalendoeditor