Pichani ni matukio mbalimbali ya ushiriki wa Wafanyakazi Wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Tamasha Maalum la uchangiaji mahitaji muhimu kwa wafungwa wanawake lililofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
………..
Wafanyakazi wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wamechangia katika ukusanyaji Fedha zitakazotumika kununua mahitaji muhimu kwa ajili ya wafungwa wanawake katika Magereza ya Keko na Segerea.
Walitoa mchango huo kupitia Tamasha Maalum lililoandaliwa na Kampuni ya Shiraz Foundation na kufanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, likilenga kukusanya Fedha kwa ajili kuwasaidia wanawake hao wenye uhitaji.
Akizungumza baada ya kushiriki katika Tamasha hilo, Mwenyekiti wa TUGHE Wanawake, Tawi la REA, Wilhelmina Cheyo ameeleza dhumuni la ushiriki na uchangiaji wao kuwa ni utamaduni waliojiwekea katika kuunga mkono jitihada za Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, kuwakumbuka na kusaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji katika jamii.
“Sisi kama akina mama, tunawiwa na tunaguswa na moyo wa upendo wa Rais wetu Mama Samia jinsi anavyoguswa na changamoto za watu mbalimbali katika jamii hivyo kwa kauli moja tumejiwekea utamaduni huu wa kutoa misaada mbalimbali kila tunapoweza kufanya hivyo ili kumuunga mkono,” amesema.
Aidha, Cheyo ameushukuru Uongozi wa REA kwa kuendelea kuwaunga mkono katika jitihada zao za kuisaidia jamii yenye uhitaji.
Mwenyekiti huyo wa Wanawake ametoa hamasa kwa Wafanyakazi wanawake katika Taasisi na Mashirika ya Serikali na Binafsi, kuwakumbuka na kuwasaidia wenye uhitaji katika jamii kwani huo ni utamaduni wa wanawake wa kiafrika wakiwa kama akina mama walezi wa jamii.
Katika kuadhimisha sherehe za Siku ya Wanawake Duniani, Machi mwaka huu, wanawake wa REA waligawa majiko na mitungi ya gesi ili kuwawezesha wanawake waishio vijijini katika Mkoa wa Dodoma, kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya kuni.