Featured Kitaifa

WAJASILIAMALI KIGOMA WAHAMASISHWA KUWEKEZA KATIKA ZAO LA MCHIKICHI

Written by mzalendoeditor

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara – Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kuhamasisha kilimo cha michikichi ya kisasa, utumiaji teknolojia bora na rafiki katika uchakataji wa zao hili ili kupata bidhaa bora, malighafi zitakazowezesha uzalishaji wenye tija na endelevu na kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Dkt. Abdallah ameyasema hayo wakati akifungua warsha ya wajasiliamali wa mnyororo wa thamani wa zao la mchikichi iliyofanyika katika ukumbi wa St. Michael Social Hall Kigoma mjini Machi 14, 2022 iliyolenga kuendeleza jitihada katika kuongeza uzalishaji na utumiaji wa zao na bidhaa za mchikichi mkoani Kigoma na Tanzania kiujumla.
Aidha, amesema Serikali imeweka mazingira bora ya kuwezesha kujenga uchumi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo ili kuongeza ajira na tija kwa wazalishaji na ubora wa bidhaa zikiwemo bidhaa za zao la michikichi kama vile mafuta ya kula aina ya Mawese, Mafuta ya mise ambayo hutumika kutengeneza sabuni, fagio, kapeti na mkaa mbadala inayotokana na mti na majani ya mchikichi.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji  akisaini Mkataba wa ujenzi wa vidogo viwili amesema SIDO iko tayari kutekeleza mradi huo katika ujenzi wa viwanda hivyo vya kukamua mafuta ya mawese katika wilaya Uvinza kijiji cha Sinuka na Wilaya ya Kigoma vijijini katika kijiji cha Nyamuhoza pamoja na kutoa mafunzo  na mikopo ya kifedha kwa wajasiliamali hao.
Naye Bi Ritta Magere Mratibu na Msimamizi wa Mradi wa EIF Tier I na II kutoka Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) – Enhanced Intergrated Framework (EIF), inatekeleza mradi wa kuongeza thamani katika zao la Mchikichi kwa kuongeza uchakataji wenye tija na ubora, kuimarisha ushindani wa biashara ndogo na za kati  katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa pamoja na kupunguza umasikini kwa kutoa ajira kwa wanawake na vijana takribani 500.
Bi Magere amesema mradi huo unatekelezwa kuanzia 2020 hadi 2023  Tanzania bara na Visiwani hasa katika mnyororo wa thamani wa mazao ya Chikichi kwa Mkoa wa Kigoma, Asali kwa Mkoa wa Singida, Mbogamboga na Matunda Kanda ya Ziwa Mikoa ya Mara na Simiyu pamoja na Dagaa Mkoa wa Unguja na Mwani Mkoa wa Pemba.
Aidha Bi Magere amesema kwa mkoa wa Kigoma Mradi huo utajenga miundombinu mbalimbali kwenye minyororo ya thamani ya mazao yaliyochaguliwa (selected value chains) kama vile kujenga viwanda vidogo vya kusindika mazao hayo, kuwezesha pembejeo kwa Wakulima kwa ajili ya kufanikisha kilimo chao, kuboresha Maabara za ubora wa bidhaa na viwango na vifaa vitakavyotumika katika  Maabara hizo,  kutoa mafunzo ya Kilimo Biashara (Farming as a Business) kwa wakulima ili kukuza kilimo chao kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi
Vilevile, amesema Mradi huo utawawezesha wakulima wa mbogamboga na matunda wa Mikoa ya Mara na Simiyu kuwa na majokofu ya kuhifadhia bidhaa (cold storage facilities) wakati wa kupelekwa bidhaa hizo sokoni, Kuwezesha wakulima wa asali kuwa mizinga ya kisasa kwa ajili ya kuvunia asali pamoja na kiwanda kidogo cha kusindika asali katika Mkoa wa Singida na kuwezesha wakulima wa mchikichi kuwa na kiwanda cha kusindika mafuta ya mawese na bidhaa zingine zitokanazo na zao la chikichi kutumika katika utengenezaji wa sabuni na mashudu ya wanyama katika Mkoa wa Kigoma.

About the author

mzalendoeditor