Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amewataka Waandishi bunifu kuwasilisha miswaada yao ili kuwania _Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu 2023_.
Prof. Mkenda rai hiyo Novemba 24, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa habari, ambapo amesema tuzo hiyo inatolewa ili kuwatambua na kuwazawadia Waandishi Bunifu pamoja na kukuza vipaji vya uandishi bunifu.
“Malengo mengine ni kukuza lugha ya Kiswahili, kukuza utamaduni wa kusoma na kujisomea, kukuza uhifadhi historia na mifano bora ya nchi, kuongeza hifadhi ya vitabu katika maktaba ya taifa, mikoa, Vyuo na shule” Alisema Prof. Mkenda.
Ameongeza kuwa, utolewaji wa tuzo hizo pia inalenga kusaidia kukuza sekta ya uchapishaji wa maandishi bora nchini Tanzania.
“Mwaka jana tuzo zilitolewa katika Riwaya na Ushairi, lakini mwaka huu zitatolewa kwenye maeneo matatu; nyanja ya Riwaya, Hadithi za Watoto pamoja na Ushairi” alibainisha Prof. Mkenda.
Amesema tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa April 13, 2024 na kwamba mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 10, pamoja na ngao ya ushindi na kwamba andiko lake litahaririwa na kuchapishwa na Wizara itanunua vitabu vyake.
Aidha amefafanua kuwa mshindi wa pili atapata shilingi milioni 7, na wa tatu shilingi milioni 5, wote kwa pamoja watapata cheti cha ushindi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu 2023 Prof. Penina Mlama amesema Kamati inaendelea kupokea miswada, na kwamba zoezi hilo litafungwa Novemba 30 2023.
“Tuliweka vigezo urefu wa Riwaya maneno 60,000 -100,000, tunategemea mashairi yasiyopungua 60 na upande wa vitabu vya watoto tunatarajia maneno yasiyozidi 1,000, kwani tunatarajia viwe na michoro zaidi” alisema Prof. Mlama.