Uncategorized

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA OFISI YA MAKAMU WA RAIS

Written by mzalendo

 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis
Hamza Khamis akifafanua jambo alipowasilisha Taarifa ya Hali ya Ufanisi katika
Uchakataji na Uandaaji wa Taarifa za Hali ya Mazingira kwa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo Oktoba 25, 2023.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Dkt. Thomas Bwana akitoa ufafanuzi wa
masuala mbalimbali wakati wa kikao cha kuwasilisha Taarifa ya Hali ya Ufanisi
katika Uchakataji na Uandaaji wa Taarifa za Hali ya Mazingira kwa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo Oktoba 25, 2023.

 

Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira na
wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwa katika Taarifa ya Hali ya
Ufanisi katika Uchakataji na Uandaaji wa Taarifa za Hali ya Mazingira kwa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo Oktoba
25, 2023.
……………………………………

Kutokana na maandalizi ya Taarifa za Hali ya Mazingira nchini, Serikali na
wadau wameweza kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhifadhi
mazingira nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akiwasilisha Taarifa ya Hali ya
Ufanisi katika Uchakataji na Uandaaji wa Taarifa za Hali ya Mazingira kwa
Kamati ya Kudumu ya Bunge jijini Dodoma leo Oktoba 24, 2023.
Amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na Taarifa ya pili
na ya tatu ya hali ya mazingira nchini kuainisha uwepo wa mikakati na
mipango mingi ya kisekta na matambuka katika hifadhi na usimamizi wa
mazingira.
”Ili kurahisisha uratibu na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa mipango na
mikakati hiyo umeandaliwa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira, 2022-2032, unaoanisha vipaumbele vya kitaifa katika kutekeleza
mipango na mikakati hiyo kwa miaka kumi. Katika maeneo ya kipaumbele
mpango huo unaonesha changamoto, visababishi vya changamoto hiyo, hatua
zilizokwisha chukuliwa, maeneo mahsusi ya vipumbele na hatua za kuchukua,”
amefafanua Mhe. Khamis.
Akiendelea kuwasilisha taarifa hiyo, amesema katika udhibiti wa uchafuzi wa
mazingira mafanikio yaliyopatikana kutokana na mapendekezo ya taarifa hizi
ni pamoja na kupiga marufuku matumizi ya vibebeo vya plastiki ambapo
takriban viwanda 70 vimeanza kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira.
Hali kadhalika, kuhifadhiwa kwa asilimia 40 ya eneo lote la nchi kwa ajili ya
makazi ya viumbe pori na bioanuai ambapo hadi kufikia mwaka 2018, jumla ya
misitu ya hifadhi asili 12 yenye ukubwa wa hekta 305,000 imehifadhiwa.
Naibu Waziri Khamis amefafanua kuwa Taarifa ya pili na ya tatu ziliainisha
uharibifu wa misitu utokanao na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa na
kufungua mashamba mapya.
”Katika kukabiliana na changamoto ya ukataji miti tumeanzisha kampeni ya
upandaji miti, ambapo kila halmashauri imeendelea kutakiwa kupanda miti
milioni 1.5 kwa mwaka kulingana na msimu wa mvua katika eneo husika. Pia,
ili kujenga msingi wa vijana wetu imeanzishwa kampeni ya Soma na Mti
ambapo kila mwanafunzi anahamasishwa kupanda mti na kuutunza awapo
shuleni,” amesema Mhe. Khamis.
Wakichangia taarifa hiyo baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Maji na Mazingira waimeipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kuratibu na

kusimamia vyema kampeni za upandaji miti ikiwemo ya Soma na Mti pamoja
na Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.
Wameshauri kuwa wanafunzi wajengewe uelewa kuhusu ni aina gani za miti
inayopaswa kupandwa katika maeneo ya shule zao zoezi hilo liwe na tija.

About the author

mzalendo