Hospitali ya Taifa Muhimbili imepokea msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya TZS. 3Mil kutoka kwa Viongozi wa Serikali ya Mtaa Kibangu iliyoko Manispaa ya Ubungo kwa lengo la kusaidia wagonjwa ambao hawana uwezo hospitalini hapo.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Bi. Redemptha Matindi ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Ukunga na Uuguzi amewashukuru kwa kuguswa na kujali kwani mahitaji ni mkubwa na si jambo jepesi kuwafikia wote.
“Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuhudumia wananchi wake lakini wahitaji ni wengi kwa hiyo sisi kama jamii tunao wajibu wa kuisaidia, pia tunawaomba wanajamii wengine wajitokeze na kusaidia wezetu” amesema Bi. Redemptha
Kwa upande Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kibangu Bw. Desdery Ishengoma amesema vitu hivi vimekusanywa kutoka kwa wananchi mbalimbali wanaoishi Kibangu na maeneo jirani ambao waliguswa na kuweza kutoa msaada huo.
“Tumeguswa na tumeona ni vyema kutoa msaada huu Muhimbili kwa wagonjwa ambao hawana ndugu hospitalini hapa ili wajisikie kama wenzao, kwani wagonjwa wa leo ndio wazima wa kesho na wazima wa leo ndio wagonjwa wa kesho” amesema Bw. Ishengoma