Baraza la Kuu la Waislam Mkoa wa wa Dar (BAKWATA) wakiongozwa na Kaimu Sheikh wa Mkoa na Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa huo Sheikh Walid Alhad Omary wamejumuika pamoja kutembelea wagonjwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuwaombea Dua, kuwafariji na kuwapa vitu kadhaa kwa ajili ya matumizi yao.
Ziara hiyo imefanyika leo kuelekea sherehe za mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) itakayofanyika Kimkoa Septemba 27 mwaka huu katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Sheikh Walid amesema katika kuelekea kuazimisha sherehe hizo, BAKWATA Mkoa wa Dar Es Salaam imeandaa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya mihadhara misikitini, kutembelea wagonjwa na kuwaombea Dua, kuchangia damu, kufanya usafi na kutoa sadaka kwa wagonjwa.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Bw. Aminiel Aligaesha amemshukuru Sheikh Walid pamoja na BAKWATA kutembelea wagonjwa, kuwaombea dua na kutoa sadaka za vitu kwao ikiwemo sabuni, miswaki, dawa za meno, pampasi n.k.
Aligaesha amesema dini ya kweli ni Ile inayowajali wahitaji hivyo walichokifanya ndicho Mwenyezi Mungu anachotaka.
Sheikh Walid ameahidi kuendelea kushirikiana na MNH katika maeneo mbalimbali ya kusaidia wagonjwa waliolazwa ili kutoa mchango wa kijamii Kwa wahitaji.