Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe, Tabia Maulid Mwita akifungua Mkutano Mkuu wa Baraza la Vijana Zanzibar hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Tabia Hall Bweleo ,14/09/2023.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdalla akiwashauri vijana kujiunga katika mafunzo ya ujasiriamali ili kuweza kujiajiri hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Tabia Hall Bweleo ,14/09/2023.
Baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Baraza la Vijana wakisikiliza kwa makini maelezo yanayotolewa na Waziri wa Wizara hiyo Mhe, Tabia Maulid Mwita(ambae hayupo pichani) katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Vijana uliofanyika Ukumbi wa Tabia Hall Bweleo ,14/09/2023.
Na Rahma Khamisi Maelezo
Waziri wa Habari, Vijana ,Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amewataka vijana kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ili kuleta maendeleo nchini.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Baraza la Vijana Zanzibar katika Ukumbi wa Tabia Hall Bweleo amesema ni vyema vijana kujishughulisha na kazi za ujasiriamali wa aina mbalimbali ili kufikia malengo ya kujiletea maendeleo.
Aidha amesema iwapo vijana watajituma na kufanya kazi kwa bidii na uzalendo watasaidia kuimarisha maendeleo yaliyopo katika jamii.
Waziri Tabia amewaasa vijana kuacha kujiingiza katika vitendo viovu ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya na badala yake kujishughulisha na kazi za mikono kwa kujiongezea kipato.
“Sisi vijana tunaangaliwa na viongozi wetu hivyo ni vyema tukasimamia yale tunayopewa ili tuweze kutatua changamoto zinazotukabili,” alisisitiza Waziri.
Ameongeza kuwa kuna miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo yanayowahusu vijana hivyo iko haja ya baraza hilo kubuni miradi hiyo ili kupata fursa za kujipatia mikopo ya kusaidia kuwawezesha vijana hao .
Waziri amefahamisha kuwa baraza la vijana ni vyema likaandaa na kupanga mikakati maalumu na kufanya maonesho makubwa yatakayotangazwa na kuonyesha kazi zao ili kuleta tija.
“Tutahakikisha kuwa tufanya kila linalowezekana kuhakikisha Baraza linafanya vizuri ili kusonga mbele ,”alifahamisha.
Aidha amelipongeza baraza la vijana kwa kufanya Mkutano huo kwani ni jambo jema ambalo litasaidia kuleta ushirikiano wa pamoja katika kujadili na kudhibitisha taarifa za Vijana na badae kutoa maazimio.
Nae Katibu Mtendaji Baraza la Vijana Salum Issa Ameir amesema katika mkutano huo kuna wajumbe 75 ambapo 71 kati yao ndio watakaopiga kura.
Amesema lengo la kuwa na vijana ni kuwasadia katika changamoto zao na kuzigeuza kuwa ni fursa kwa kuwaunganisha pamoja kupitia makundi mbalimbali.
Amefahamisha kuwa katika mkutano huo watafanya kazi mbili ikiwemo kudhibitisha na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu vijana.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Khamisi Abdalla amesema Wizara imejipanga katika kuwaendeleza Vijana ili waweze kujiajiri wenyewe kupitia miradi mbalimbali waliyoianzisha.
Amesema Serikali itajenga Vyuo vitano vya amali katika kila Mkoa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kwa kuwapatia elimu na kuwajengea uwezo.
Mwenyekiti Baraza la Vijana ameomba wizara kupatiwa posho kwa wenyeviti wa Wilaya wakati utaporuhusu angalau kujisaidia