Featured Kitaifa

BILIONI 24 KUBORESHA HUDUMA MBALIMBALI HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA DODOMA

Written by mzalendoeditor

 

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dk.Ernest Ebenzi,akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 9,2023 jijini Dodoma  kuhusu utekelezaji wa majukumu na vipaumbele vya hospitali hiyo kwa mwaka 2023/2024

Waandishi wa habari wakimsikiliza Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dk.Ernest Ebenzi,wakati akitoa taarifa  leo Agosti 9,2023 jijini  Dodoma  kuhusu utekelezaji wa majukumu na vipaumbele vya hospitali hiyo kwa mwaka 2023/2024

Na Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imeitengea sh.Bilioni 24  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa mwaka fedha  2023/2024 ili kuboresha huduma  kwa wananchi kwa gharama ndogo  na kuhakisha  dawa zinapatikana kwa wakati na  za kutosha.

Hayo yamesemwa leo Agosti 9,2023 jijini Dodoma na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dk.Ernest Ebenzi,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu na vipaumbele vya hospitali hiyo kwa mwaka 2023/2024

”Katika mwaka huu wa fedha wa 2023/2024 tumetengewa Shilingi bilioni 24 ili kuendelea kuwahudumia wananchi kwa wakati na huduma bora kwa gharama ndogo, kutumia muda mfupi katika kumuhudumia mgonjwa pamoja na uhakika wa dawa za kutosha na kuendelea kukarabati na kujenga majengo kwa ajili ya kutolea huduma mbalimbali za afya.”amesema Dkt,Ebenzi

Dkt,Ebenzi amesema kuwa Hospitali inaendelea kukarabati na kujenga majengo kwa ajili ya kutolea huduma mbalimbali za afya ikiwa ni Pamoja na kuendelea kupiga hatua katika kutoa huduma bora kwa kuzingatia sayansi na teknolojia ya kisasa.

“Tunaendelea kufanya tafiti mbalimbali, kuwasomesha watumishi wa hospitali,kujenga jengo la gorofa 5 kwa ajili ya sehemu mbalimbali za kutolea matibabu,Kuboresha mikakati ya ukusanyaji damu na kuendelea kuboresha na kujenga miundombinu ya hospitali kwa ujumla,”amesema Dk.Ebenzi

Amesema kuwa Kutokana na maboresho ya Sekta ya Afya nchini,Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma
inapokea wagonjwa zaidi ya 1,500 kwa siku na uwezo wa kulaza wagonjwa 250 hadi 350 kwa wakati mmoja.

Ameeleza kuwa kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 Idara ya magonjwa ya nje na dharura ilihudumia wagonjwa 251,174, wagonjwa 13,607 kwa utaratibu wa rufaa, 120,263 (48%) walitibiwa kwa bima ya NHIF na 8,174 (3%) walikuwa wa bima nyingine huku wagonjwa 16,896 (7%) walikuwa wa CHF, na 105,841(42%) walipata huduma kwa njia nyingine za uchangiaji ikiwemo wa msamaha.

Dk.Ebenzi ameeleza kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja yaani 2022/2023 Hospitali ilifanikiwa kufanya Kliniki tembezi katika maeneo tofauti ndani ya Mkoa wa Dodoma ambapo wagonjwa 552 walihudumiwa.

“Katika kipindi cha mwaka 2022/2023 Idara ya Macho ilifanikiwa kutoa huduma kwa wagonjwa 5,319, wagonjwa waliofanyiwa upasuaji 2,234, wagonjwa 843 walipatiwa dawa aidha kwa mwaka 2022/2023 Idara ya famasia imehudumia jumla ya wagonjwa 183,664, kati yao wagonjwa 83,583 walikuwa wa Bima na 100,081 wa kujitegemea,”ameeleza

Amesema wastani wa mahitaji ya damu kwa mwaka Hospitali ya Rufaa ya Dododma ni chupa/units 5,400, kipindi cha mwaka 2022/2023 chupa/Units 5,368 zilikusanywa sawa na asilimia 99% aidha, hakuna mteja aliyekosa damu.

Akizungumzia kitengo cha uchunguzi kwa njia ya mionzi (Radiolojia) kwa mwaka 2022/2023, amesema kilifanikiwa kufanya jumla ya vipimo 37,975 vya aina mbalimbali na kwamba Hospitali hiyo imefanikiwa kununua vifaa tiba vya kisasa ikiwemo CT- Scan, X- Ray mashine 3 za kisasa zaidi kutoka mashine 1.

Ametaja vifaa vingine kuwa ni mashine za Ultrasound 4, mashine za kisasa za maabara na vitendanishi, na kufanya vipimo 136 vinavyosaidia wananchi kutambua changamoto mbalimbali za afya zao.

Kwa upande wa tiba,Dk.Ebenzi amesema “tunao madaktari bingwa wa upasuaji, mifupa, uzazi kwa kina mama na mtoto, meno, macho, pua, koo na sikio, magonjwa ya ndani, ngozi na magonjwa ya zinaa,tunatoa huduma ya kliniki tembezi za kibingwa kwa wananchi pamoja na kuwajengea uwezo wa kitaalamu watumishi walio katika vituo vya ngazi ya chini,”amesema

Ameeleza kuwa huduma za kinga hutolewa kwa kutoa chanjo kwa wateja waliolazwa na wanaofika kupata huduma za nje (OPD), chanjo hizo ni chanjo zote za awali kwa watoto, chanjo za wajawazito, chanjo za pepopunda (Tetenus), homa ya ini, manjano, UVIKO-19 na chanjo dhidi ya kichaa cha wanyama.

Akieleza changamoto zinazoikabili Hospitali hiyo amesema ilikuwa na ufinyu wa jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje na dharura ambalo lilikuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 4 tu wa dharura kwa wakati mmoja na kueleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imefanya mabadiliko makubwa katika uboreshaji wa jengo ya dharura ambapo wagonjwa 34 wanapata huduma za uchunguzi, vipimo na malipo ya huduma kwa wakati mmoja na uharaka zaidi kulinganisha na hapo awali .

“Jengo la kuwahudumia wagonjwa walio kwenye uangalizi maalum (ICU lina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 38 ukilinganisha na wagonjwa wa 3 waliohudumiwa katika jengo la zamani, na lina vifaa vya kisasa ikiwemo vitanda vyote kuwageuza wagonjwa kwa kutumia umeme,”amesema.

About the author

mzalendoeditor