Na WMJJWM, Mbeya.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema umefika wakati Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na ustawi wa Jamii, (SMAUJATA) kueneza Kampeni hiyo Visiwani Zanzibar ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kupambana na vitendo vya ukatili.
Mhe. Mwanaidi ameyasema hayo Agosti 07, 2023 wakati alipokuwa akitembelea Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea mkoani Mbeya katika Viwanja vya John Mwakangale.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum itaratibu safari ya baadhi ya Wawakilishi wa SMAUJATA kwenda kuamsha ari ya kupambana na vitendo vya ukatili Zanzibar ili mapambano hayo yawe na sura pana ya kitaifa.
“SMAUJATA kwakweli kwa upande wa bara mnafanya vizuri sana ninatamani kuona hiki mnachokifanya huku mkipeleke na Zanzibar kuamsha amsha ili Jamii ya Wazanzibar iwe na muamko zaidi katika kupambana na vitendo vya ukatili” amesema Mhe. Mwanaidi
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mwanaidi amelipongeza Baraza la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi huku akiulekeza uongozi wa Baraza hilo Mkoa wa Mbeya kushirikiana na uongozi ngazi ya Taifa kuwawezesha wanawake wa mkoa huwa wanaojishughulisha na shughuli za Ufumaji kwenda kwenye maonesho ya kimataifa nchini Burundi kwani kuna uhitaji wa bidhaa za ufimaji.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo ya Naibu Waziri Mwanaidi, Mwenyekiti wa Baraza hilo Taifa Fatuma Kange amesema wanatambua mchango mkubwa unaotolewa na Serikali katika kuwawezesha wanawake wajasirimali katika kupata mikopo na masoko ndani na nje ya Tanzania kwaajili ya kuuza bidhaa zao.
“Mhe Naibu Waziri sisi tunathamini sana mchango wa Serikali, mpaka sasa nchi nzima tuna Mabaraza haya ambayo yametusaidia kufahamiana na kubadilishana uzoefu lakini kupeana fursa za maeneo tofauti tofauti” amesema Fatuma.
Banda la Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Taasisi na wadau wake mbali na kupokea ugeni wa Naibu Waziri, Katibu Mkuu vile vile ilipata bahati ya kutembelewa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda ambaye aliipongeza Wizara na Taasisi zake kwa jinsi zinavyoonesha ubunifu kwenye kozi mbalimbali zinazotolewa katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini.