Na WMJJWM, Mbeya
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amepongeza jitihada zinazofanywa na Wanawake Wajasiriamali kutoka Mabaraza ya Uwezeshaji wanawake kiuchumi kote nchini kutokana na ubunifu wanao ufanya katika bidhaa wanazozalisha.
Dkt Jingu ameyasema hayo alipotembelea Banda la Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Wadau wake katika maonesho ya wakulima Nanenane yanayofanyika Kitaifa mkoani Mbeya.
Dkt. Jingu amesema, shabaha ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na wadau wake kushiriki maonesho hayo ni kuonesha kile wanachokifanya lakini pia kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali yahusuyo Maendeleo na Ustawi wa Jamii.
“Kwa sasa bidhaa nyingi za wajasiriamali wetu ni nzuri ambazo zinatuwezesha kushindana hata kimataifa, hivyo tunapokuja kwenye maonesho ni katika hali ya kubadilishana uzoefu” amesema Dkt. Jingu.
Aidha DktJingu amesema Wizara itaendelea kushirikiana na wajasiriamali walioinuka na wanaochipukia ili kila mmoja aone fahari ya uwepo wa Wizara hiyo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Jingu ameendelea kuwahimiza watu wa kada zote kupinga ukatili kwani uwepo wa ukatili ni kikwazo katika kufikia maendeleo endelevu na usawa wa kijinsia.
“Wenzetu hawa SMAUJATA wanafanya kazi kubwa sana ya mapambano dhidi ya ukatili rai yangu tuwaunge mkono, wenyewe peke yao hawataweza tukiunganisha nguvu tutaweza kwa pamoja” amefafanua Dkt. Jingu.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inashiriki kwa mara ya pili maonesho ya Wakulima Nane Nane yanayoendelea mkoa Mbeya yanayoongozea na kauli mbiu isemayo. “Vijana na Wanawake ni msingi imara wa mfumo endelevu wa chakula”.