Featured Kitaifa

RC SENYAMULE :FANYENI KAZI KWA WELEDI KWA KUZINGATIA MAADILI 

Written by mzalendoeditor
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na wahitimu wa Taasisi ya Afya na Sayansi Shirikishi (DIHAS) na kuwaasa kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia maadili na miiko ya taaluma waliyoipata kwa kuthamini utu kwa wagonjwa wataokuwa wanawahudumia. Senyamule ameyasema hayo katika mahafali ya 39 ya Chuo hicho yaliyofanyika Jijini Dodoma
Na.Mwandishi Wetu-DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewaasa wahitimu wa Taasisi ya afya na Sayansi Shirikishi (DIHAS) kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia maadili na miiko ya taaluma waliyoipata kwa kuthamini utu kwa wagonjwa wataokuwa wanawahudumia sambamba na kuzingatia mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia kwa kuendelea kutafuta elimu.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo Julai 28,2023 wakati akitoa hotuba yake kwenye mahafali ya 49 ya Chuo hicho iliyofanyika katika Viwanja vya Chuo hicho. 
“Wahitimu nawaasa kokote muendako katika kuwatumikia wananchi, mfanye kazi kwa weledi mkizingatia maadili na miiko ya taaluma mliyoipata, mkathamini utu wa wale mtakaokuwa mkiwahudumia, muwe raia wema na watendaji wanaofuata sheria, epukeni rushwa, ufisadi na mjikinge na ugonjwa hatari wa ukimwi. Zingatieni pia mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia kwa kuendelea kutafuta elimu. Elimu ni uhai, haina mwisho na tunu ambayo ukipata hakuna atakayekupokonya “amesema Senyamule 
Aidha, Mhe. Senyamule amewataka wahitimu hao kutumia maarifa waliyo yapata kutoa elimu kwenye jamii wanazoenda ili kuwasadia kujikimu kwenye maisha yao ya kila siku na kutosubiri ajiraa za Serikali. 
Katika hatua nyingine, Mhe.Senyamule amewapongeza Wazazi na Walimu kwa kugharamia ada za mafunzo kwa watoto wao. Pia amewashukuru wafanyakazi na wanajumuiya wote wa Taasisi hio kwa kuendelea kufanya  kazi kwa bidii.
Kwa Upande Wake, Bi. Upendo Kilumbe Mkuu wa Taasisi ya Afya na Sayansi Shirikishi Dodoma (DIHAS) ametaja jukumu kuu la chuo hicho kuwa ni kutoa mafunzo yaliyo bora na yanayozalisha wahitimu wenye weledi wakutosha hivyo wataendelea kuboresha huduma za mafunzo ikiwemo kuendelea kutoa  ujuzi kwa wakufunzi ili waendelee kutoa elimu bora zaidi kwa wanafunzi.
Katika Mahafali hiyo Mhe. Senyamule ameahidi kutatua baadhi ya changamoto alizoelezwa na uongozi wa Chuo hicho na kuahidi kushirikiana na Wizara ya Afya na Taasisi mbalimbali katika kuboresha miundombinu ya mafunzo kwa vitendo, kujenga maeneo ya kujisomea wanafunzi na kuahidi kuendelea kushirikiana katika mbalimbali baina ya Ofisi yake na Chuo hicho.

About the author

mzalendoeditor