Featured Kitaifa

KATAMBI AAGIZA MAMENEJA WA MIFUKO KUMALIZA MALALAMIKO YA WASTAAFU

Written by mzalendoeditor

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (Mb) akijibu swali Bungeni leo tarehe 19 Juni, 2023, jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

Serikali imewaagiza Mameneja wa mifuko ya hifadhi ya jamii wa Mikoa kuhakikisha hakuna malalamiko ya wastaafu kwenye maeneo yao kwa kuwa hicho kitakuwa kipimo cha utendaji kazi wao.

Aidha, hadi sasa wastaafu wote wa serikali wameshaboreshewa pensheni zao za kila mwezi.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameyasema hayo bungeni Juni 19, 2023 alipokuwa akijibu maswali ya ya wabunge na kupokea maelekezo ya Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson kuhusu waajiri wasiopeleka michango ya waajiriwa kwenye mifuko na kusababisha kutopata mafao yao kwa wakati pindi wanapostaafu.

Mhe.Katambi amesema “Nimechukua na kupokea mwongozo wako (Spika), nitumie nafasi hii kwa sababu hatua zimeshachukuliwa ikiwemo kuwafikisha mahakamani, wakati mwingine mashauri yanachelewa lakini sasa tutachukua hatua kwa mameneja wa mikoa ili kama hawezi kuwahudumia watanzania basi waje wengine wanaoweza kuwahudumia.”

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti maalum (CCM), Mhe. Adam Malembeka amehoji serikali itaongeza mafao kwa askari wastaafu.

Naibu Waziri katambi amesema kanuni ya ulipaji mafao Namba 11(1) za mwaka 2018 zilielekeza Mfuko wa PSSSF kuongeza pensheni kwa kuzingatia mfumuko wa bei na uendelevu wa Mfuko kila baada ya miaka mitatu.

About the author

mzalendoeditor