Featured Kitaifa

MAREKANI KUTOA FEDHA ZAIDI KUPAMBANA NA UKIMWI

Written by mzalendoeditor

OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki amesema Serikali ya Marekani kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR) imetenga dola za Marekani milioni 450 kwa ajili ya kutekeleza afua mbalimbali za afya ikiwamo kupambana na UKIMWI.

Pia amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Marekani katika kutekeleza afua za kupambana na UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria.

Kairuki ameyasema hayo jijini hapa wakati wa ziara ya timu ya viongozi kutoka mpango wa dharura wa kupambana na UKIMWI (PEPFAR), Programu ya UNAIDS na Global fund.

Alisema pia PEPFAR imeahidi kutenga dola za Marekani milioni 450 kwa mwaka 2023 ambazo zitatumika kati ya Oktoba 2023 hadi Septemba 2024 kwa ajili ya afya ikiwemo, kupambana na UKIMWI, kuimarisha mifumo ya afya na uzazi wa mpango.

“Ofisi ya Rais-TAMISEMI inathamani ziara hii ambayo inasaidia kuimarisha ushirikiana kati ya Serikali ya Tanzanua na Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR.”

Alisema Serikali inatekeleza afua mbalimbali za afya katika maeneo ya msingi ya VVU/UKIMWI, Kifua kikuu, Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto; Uzazi wa Mpango, lishe, Malaria, Magonjwa ya Kitropiki yasiyopew kipaumbele na kuimarisha mifumo ya afya.

Kairuki alisema ikiwa PEPFAR inaadhimisha miaka 20 tangu kuanza ufadhili wake hapa nchini mwaka 2003, Serikali ya Marekani imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya UKIMWI ambapo takribani dola za Marekani bilioni 6.6 zimewekezwa kwenye afua ambalimbali za afya.

Alisema Tanzania, kuna vituo vya afya vya umma na binafsi vilivyosajiliwa 8,796 na kati ya hivyo 6,893 vinatoa huduma kamili za VVU chini ya msaada wa PEPFAR na asilimia 90 ya vituo hivyo vinatoa hduma ya afyamsingi.

Kairuki alisema wakati PEPFAR inaanza kusaidia Tanzania mwaka 2004, watu 500 wanaoishi na VVU ndio waliokuwa wanapata huduma kamili za VVU katika vituo vya afya na kwa sasa watu milioni 1.6 wanapata matibabu ya bure ya dawa za kurefusha maisha.

Alisema juhudi hizo zimesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa asilimia 76 wakati maambukizi mapya yakipungua kwa asilimia 58.

“Tunashukuru kwa msaada wa PEPFAR katika kusaidia katikakuimarisha mfumo wa afya, kuziba pengo la rasilimali watu kwa ajili ya afya, kuimarisha uwezo wa maabara, kuimarisha mifumo ya taarifa za afya, na kushiriki katika ufuatiliaji wa magonjwa, utafiti na tathmini ya afua za afya.

“Pia tunatambua msaada wa PEPFAR katika kupanua huduma za uzazi wa mpango, na mapambano dhidi ya magonjwa ya milipuko.”

Kwa upande wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Tanzania haijafanya vizuri kwenye lengo la kujua hali ya maambukizi ambayo kwa sasa ni asilimia 86 chini ya lengo la kidunia la asilimia 95 na kuwa hilo linachangiwa na mwitikio mdogo wa wanaume kutopima afya zao.

Alisema ili kuendelea kufanya vizuri, Wizara ya afya imeweka mikaka ya kuhakikisha idadi ya wananchi wanaojua hali zao inaongezeka na kuzuia maambukizi mapya ya VVU kwa wasichana balehe ambao ndio waathdirika wakubwa.

“Pia tunakwenda kupambana na suala la maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambalo bado kama nchi hatujafanya vizuri.”

Mratibu wa PEPFAR na Mwakilishi Maalum wa serikali ya Marekani katika masuala ya Diplomasi ya Afya, Balozi Dk.John Nkengasong aliipongeza Serikali kwa kusimamia utekelezaji wa afua za afya amabo imetokana na uongozi shupavu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Naye Mwakilishi Maalumu wa Global Heath Diplomacy na Makamu Mkurugenzi Mtendaji wa masuala ya program wa UNAIDS, Angeli Achrekar alisema wamefurahishwa na kuona jinsi Tanzania imefanya kisichowekezaka katika kusimamia afua za afya.

About the author

mzalendoeditor