Featured Kitaifa

KAMATI YA WAZIRI MKUU YAANZA KUKUSANYA MAONI YA WAFANYABIASHARA DAR ES SALAAM

Written by mzalendoeditor

Kamati maalum ya kutatua changamoto za kibiashara nchini iliyoundwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa imeanza kukusanya maoni ya wafanyabishara kutoka sekta mbali mbali jijini Dar Es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt.John Jingu amesema kuwa kamati hiyo imepewa siku 14 kukamilisha kazi ya kukusanya maoni ya wafanyabishara kote nchini na kuwasilisha Taarifa hiyo Serikalini kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.

Dkt. Jingu amepongeza mahudhurio ya wafanyabiashara hao na namna wanavyotoa maoni yao kwa uwazi na uhuru kwa ajili ya kuwezesha pande zote mbili kufikia muafaka wa kutatua changamoto zilizojitokeza hapo awali na kupelekea wafanyabiashara kufunga maduka yao ikiwa ni njia mojawapo ya kufikisha maoni yao.

‘’Natoa shukrani zangu za dhati kwa Wafanyabiashara wa Dar es Salaam kwa kutuunga mkono na kutupa ushirikiano wa hali ya juu, hivyo natoa wito kwa Wafanyabiashara watakaopitiwa na kamati hiyo kote nchini kutoa ushirikiano kwa kamati ili kuwezesha kupatikana kwa majawabu sahihi na kuleta mapendekezo yanayotakiwa’’
aliongeza Dkt. Jingu.

Kwa upande wake katibu wa kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Dr. Hashil Abdalah amesema kuwa Serikali ya Dkt. Samiah Suluhu Hassan ni sikivu hivyo ipo tayari kuwapatia Wafanyabiashara hao nafasi ya kujadili kwa pamoja kero zao ili kuona nini kifanyike na kupata ufumbuzi yakinifu.

‘’Niwaahidi Watanzania, Mhe. Rais yupo tayari kuwasaidia Wafanyabiashara wote kwani ameonesha nia kubwa na kuguswa zaidi na matatizo yaliyojitokeza na kusababisha mgomo na ndio maana ameituma kamati hii ili kusikiliza kero na kisha kuziwasilisha serikalini kwa maslahi mapana ya nchi na kudumisha uhusiano uliopo baina ya Serikali na Wafanyabiashara nchini.’’
alisisitiza Dr.Hashil.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Bw. Hamis Livembe alisema kuwa Kikao hicho ni kwa ajili ya kupata Mapendekezo ya nini kifanyike ivyo amewashauri Wafanyabiashara kutoa maoni na kero zao zote zinazowakabili ili Serikali iangalie namna bora ya kuweza kuwasaidia.

Kamati hiyo inayoundwa na wajumbe 14 kutoka kwa wawakilishi wa wafanyabiashara, Wizara na Taasisi mbalimbali zinazohusika na biashara nchini, imepanga kufanya mikutano kwa siku mbili kuanzia tarehe 22 na 23 Mei, 2023 Jijini Dar Es Salaam, kisha itahamia katika kanda mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar na kuhitimisha kwa kufanya majumuisho kabla ya kuwasilisha ripoti hiyo Ofisi ya Waziri Mkuu.

About the author

mzalendoeditor