Featured Kitaifa

SERIKALI KUKABIDHI AMBULANCE MPYA 316 KWA HALMASHAURI ZOTE NCHINI.

Written by mzalendoeditor

OR TAMISEMI

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo J. Dugange(Mb) amesema Serikali katika mwaka wa fedha 2022/23 imetenga shilingi bilioni 35.1 kwa ajili ya ununuzi wa magari 316 ya kubebea wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Amesema hayo leo tarehe 24 Aprili 2023 Bungeni Dodoma wakati akijibu Swali la Mbunge wa Jimbo la Mfindi Kusini, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile aliyetaka kujua Je, ni lini Serikali itapeleka magari ya kubebea Wagonjwa katika Vituo vya Afya vya Mtwango na Mgololo.

Dkt. Dugange amesema taratibu za manunuzi zinaendelea na magari hayo yatagawiwa kwenye Halmashauri zote 184 ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ambayo itapewa magari 2 ya kubebea wagonjwa.

Amesema Serikali inatambua umuhimu na uhitaji wa magari ya kubebea wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Kadhalika, Wakati akijibu swali la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Dkt. John Danielson Pallangyo aliyetaka kujua Je, kuna mpango gani wa kukarabati miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Arumeru.

Dkt. Dugange amesema Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali Kongwe nchini na Katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23 Serikali imetenga fedha Shilingi Bilioni 17.1 kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali 19.

Aidha, Dkt. Dugange amesema hadi kufikia mwezi Februari, 2023 kiasi cha shilingi bilioni 12.95 zimekwishatolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya hospitali Kongwe 14.

Amesema katika Mwaka wa Fedha wa 2023/24 Serikali itatenga Shilingi Bilioni 27.9 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe 31 ikiwepo hospitali ya Halmashauri ya Meru ambayo imetengewa Shilingi Milioni 900.

About the author

mzalendoeditor