Featured Kitaifa

SERIKALI KUENDELEA KUTOA MAFUNZO YA UZOEFU KAZINI KWA VIJANA-WAZIRI NDALICHAKO

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akijibu swali leo Bungeni katika Mkutano wa 11 wa Bunge kikao cha 12 Aprili 24, 2023 jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof.Joyce Ndalichako, amesema serikali imeendelea kuwapatia mafunzo ya uzoefu kazini vijana ikiwamo wanaohitimu masomo yao nje ya nchi.

Ofisi hiyo kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira (TAESA) kimekuwa kikiratibu utoaji wa mafunzo ya uzoefu kazini kwa vijana wakati wakisubiri ajira.

Prof.Ndalichako ameyasema hayo Aprili 24, 2023 alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Fakharia Shomar Khamis.
Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji serikali inawatengenezea mazingira gani vijana waliofadhiliwa masomo nje ya nchi pindi wanapohitimu ili waishi maisha bora.

Akijibu swali hilo, Mhe. Waziri Ndalichako amelihakikishia Bunge serikali imeendelea kutoa ajira kupitia sekretarieti ya ajira na sekta binafsi ambayo inakua kwa kasi kubwa huku ikitengeneza mazingira ya kuwapatia mafunzo ya uzoefu kazini.

About the author

mzalendoeditor