Kaimu Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Kijamii, Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Judith Ngoda (kulia) akimuelezea Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Dkt. Aziz Mlima (hayupo pichani) kuhusu Mkutano wa Tano Baraza la Mawaziri la kisekta la Uvuvi Ukuzaji Viumbe Maji la Jumuiya ya Afrika Mashariki waliofika Ubalozini kumpa taarifa kuhusu mkutano huo unaoendelea jijini Kampala, Uganda, kushoto ni Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Didas Clemence. |
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Dkt. Aziz Mlima ameisihi sekta ya uvuvi nchini kuangalia namna ya kufanya ili juhudi za ukuzaji viumbe maji zisambae nchi nzima.
Mhe. Balozi Mlima ametoa rai hiyo jijini Kampala alipozungumza na washiriki wa Mkutano wa Tano Baraza la Mawaziri la kisekta la Uvuvi Ukuzaji Viumbe Maji la Jumuiya ya Afrika Mashariki waliofika Ubalozini kumpa taarifa kuhusu mkutano huo unaoendelea jijini Kamapala.
Akizungumza na wataalamu hao Mhe. Balozi Dkt. Mlima amesema sekta ya Uvuvi kupitia eneo la ukuzaji viumbe maji lazima ihakikishe programu za ufugaji samaki zinaenea katika maeneo mengine yenye maziwa na isiishie maeneo ya Ziwa Victoria pekee ili nchi itumie fursa hiyo vizuri na kunufaika nayo.
“Tanzania tuna eneo kubwa la maji lakini ufugaji wa samaki kwetu sio mzuri Inabidi tuoneshe njia, suala hili linatoa ajira na lina soko kubwa niwaambie tu kuwa bidhaa zitakazozalishwa soko liko DRC,” alisema na kuongeza kuwa Tanzania lazima kufanya ufugaji samaki kuwa suala la kimkakati.
Amesema kinachotakiwa kufanywa au kuangaliwa ni suala la kuzalisha chakula cha samaki ili kuwa na uhakika wa malisho yao na hapo mambo yataenda vizuri kwani suala la kutengeneza chakula ni kubwa na ana hakika chuo cha uvuvi na Taasisi ya Utafiti ya uvuvi wanaweza kusimamia eneo hilo.
Amesema sekta inabidi ioneshe njia na kutilia mkazo suala la ufugaji wa samaki nchini kwani ajira nyingi zitatengenezwa katika eneo hilo na kwa kuzingatia kuwa kuna soko kubwa kwa nchi jirani ya DRC na hivyo nchi itanufaika na fursa hii kuwa na mashine za uhakika za uzalishaji wa chakula cha Samaki
“Tuangalie na tufanye suala hili kimkakati hasa katika eneo la kutengeneza chakula cha samaki ni suala kubwa na la msingi, nina hakika chuo cha uvuvi na taasisi ya utafiti wakilisimamia hili tutapata mitambo ya kuzalisha chakula cha samaki.
Amesema anaona ufugaji Samaki ukizingatia masharti na vigezo vyake ni kitu rahisi kwa mwananchi kufanya kwakua changamoto pekee inayoweza kumsumbua mfugaji husika ni wizi wa mazao yake tu na kwamba akijipanga kudhibiti hilo hakuna shida nyingine kama ana uhakika wa chakula bora.
Mhe.Balozi Dkt. Mlima atashiriki katika Mkutano huo utakaofanyika tarehe 19 Aprili akimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo utaongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo Prof. Riziki Shemdoe kwa ngazi ya Makatibu Wakuu.