Akizungumza kwenye hafla fupi ya futari iliyoandaliwa na benki ya NBC kwa ajili ya wateja wake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Dkt Kikwete pamoja na kuipongeza benki hiyo kuwa karibu na wateja wake, alionyesha kuridhishwa na uimara wa taasisi za fedha nchini kwasasa huku akitolea mfano benki hiyo ya NBC inayomiliki mali (Assets) zenye thamani ya TZS 1.52 trilioni na amana (Deposits) zenye thamani ya TZS 1.96 trilioni.
“Mnapoandaa matukio kama haya mnaongeza imani kwa wateja wenu kwa kuwa mnathibitisha namna mlivyo nao pamoja. Hata hivyo nafarijika pia kuona mnaendelea kufanya vizuri kiutendaji kwa maana idadi ya matawi yenu inaongezeka sambamba na idadi ya mawakala wenu ambao kwasasa wamefika 9,430 nchini nzima. Mmeendelea kubuni huduma zinazowagusa wananchi wa makundi yote wakiwemo wafanyabiashara na wakulima hongereni sana,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Dkt Kikwete uimara wa taasisi za fedha nchini kwasasa utasaidia zaidi ukuaji wa uchumi kwa kuwa wawekezaji kwenye sekta ya biashara na kilimo wanategemea zaidi taasisi hizo ili kufanikisha uendeshaji wa miradi yao.
“Hakuna uchumi bila uwekezaji kama ambavyo pia hakuna uwekezaji bila mikopo ya uhakika kutoka taasisi za kifedha. Nawasihi sana benki ya NBC na taasisi nyingine za kifedha muendelee kuwa karibu na wawekezaji kwa faida ya ukuaji wenu kama wakopeshaji, pia na kwa faida ya wawekezaji wenyewe, jamii pamoja na serikali kwa ujumla,’’ alisisitiza.
Awali akizungumzia hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi, alisema ni muendelezo wa utaratibu wa benki hiyo kwa miaka 9 sasa ikilenga kujumuika na wateja wake kama hatua ya kuonyesha mshikamano na umoja katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema benki hiyo inaheshimu sana Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kutokana na ukweli kwamba, ni kipindi ambacho mwanadamu anajiweka karibu na Muumba wake kupitia mfungo na kufanya maombi.
“Huu ni mwezi ambao pia unatukumbusha kufanya kilicho chema mbele za Mungu wetu. Kwa kuwa NBC siku zote tupo karibu imani za wateja wetu tumeamua kuandaa futari hii ili kujumuika na wenzetu kufanikisha hilo.” Alisema Sabi.
Zaidi alibainisha kuwa benki hiyo ina huduma maalum inayojikita katika kutoa huduma kwa wateja wake wa imani ya Kiislam, yaani Islamic Banking inayopatikana kwenye matawi yote ya benki hiyo ikiendeshwa katika misingi ya dini hiyo ikiwa na huduma mbalimbali ikiwemo akaunti ya La Riba.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw Amosi Makalla, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw Edward Mpogolo aliipongeza benki hiyo kwa mchango wake katika kuinua uchumi wa mkoa huo kwa kuwa karibu zaidi na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara pamoja na program zake mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii (CSR).
“Kama mkoa tunafurahishwa zaidi kuona kwamba taasisi za fedha zinaheshimu imani za kidini za wateja wao sambamba na kuwa karibu zaidi na viongozi wa dini. Matunda na hatua hii ni pamoja na amani ambayo ndio msingi wa ustawi wa biashara na uchumi,’’ alisema Mpogolo.
Hafla hiyo ya futari ilihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, wateja, mawakala pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo.