Featured Michezo

TANZANIA YAANZISHA ZAO JIPYA LA UTALII-MHE. MCHENGERWA

Written by mzalendoeditor
 
Na John Mapepele
 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema katika kukuza zao jipya la utalii wa kihistoria Serikali imeanzisha mfumo wa kisasa wa kidigitali wa kusajiri mikusanyo ya malikale utakaosaidia wageni kuona maonesho mbalimbali ya kidigitali wakiwa sehemu yoyote dunia.
 
Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Aprili 5, 2023 na kufafanua kuwa Serikali imeboresha zao hilo jipya la utalii wa kihistoria ambalo linatarajia kuvuta watu wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani ambapo hadi sasa tayari asilimia 80 ya mikusanyo imeshasajiliwa kwenye mfumo.
 
Amesema kuwa mfumo huo umewekwa kwenye makumbusho ya taifa jijini Dar es Salaam ambapo pia wageni wanaotembelea makumbusho ya taifa wanaweza kuingia na kutazama maonesho ya kidigitali ya mila na tamaduni za kitanzania kama vile historia ya mtu wa kale; zamadani na mambo mbalimbali.
 
Amefafanua kuwa gharama za kutembelea na kujionea utalii huu nchini ni nafuu ukilinganisha na nchi nyingine.
 
Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na historia kubwa kutokana na makabila zaidi ya 120ambayo mila zao zinafanya kupatikana kwa utalii wa utamaduni.
 
Aidha, amesema utalii wa Tanzania umefunguka kwa kasi katika kipindi hiki kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri wa Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia Filamu aliyoifanya ya Royal Tour.
 
Ameongeza kuwa ujenzi wa mnara wa kumbukizi ya mlipuko wa mabomu ya ubalozi wa Marekani katika Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam na ziara ya kihistoria ya Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris na kuweka taji la maua kwenye mnara huo alipotembelea Tanzania hivi karibuni umesaidia kuongeza idadi ya watalii wanaopenda kujua historia mbalimbali.
 
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga amethibitisha kuwa kutokana na ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani kumekuwa na wimbi kubwa la wageni kuja kutembelea na kujionea mnara huo.
 

About the author

mzalendoeditor