Dar es salaam
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Kampuni ya Nyati Mineral Sands Ltd kuanza kulipa fidia wananchi wapatao 1,200 wa Kigamboni waliopisha eneo la mradi wa uchimbaji wa madini mazito ya mchanga wa baharini (Heavy Mineral Sand).
Dkt. Kiruswa amesema maeneo hayo yalishafanyiwa tathmini tangu mwezi septemba mwaka 2020 na kampuni ikaahidi kulipa fidia kabla ya Desemba 2022.
“Malalamiko ya wananchi wanaotakiwa kulipwa fidia yameongezeka baada ya kuahidiwa kulipwa fidia mwaka 2020. Hadi sasa bado hawajalipwa na mwekezaji hajaeleza watalipwa lini,” amesema Dkt. Kiruswa.
Aidha, Dkt. Kiruswa ameiagiza kampuni hiyo ya Nyati kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji huo mapema ili mchakato wa ulipwaji wa fidia uanze mara moja na kusisitiza zoezi hilo liendeshwe haraka ili kuondoa malalamiko ya kampuni hiyo kwa wananchi juu ya uchelewaji wa fidia.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Kampuni ya Strandline Resources Ltd (kampuni mwenza wa Nyati) Jamie Cann, ameeleza mchakato wa ulipwaji fidia umeanza kwa wahusika waliopisha mradi huo.
Amesema, jumla ya Dola za Marekani Milioni 8.5 zimetengwa na kampuni kwa ajili ya kulipa fidia wananchi.
“Kila mnufaika atalazimika kufungua Bank akaunti chini ya usimamizi na wameazimia iwe benki ya NMB, tutatoa mafunzo kwa wanufaika juu ya utunzaji fedha na uendelevu na kumsainisha mkataba kila mnufaika mkataba wa maridhiano,” ameeleza Cann.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es salaam Ally Maganga.