Uncategorized

RC SENYAMULE ATAKA WANAWAKE KUSIMAMA KATIKA NAFASI ZAO

Written by mzalendoeditor

 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza katika Kongamamo na ibaada ya maombi ya wanawake dunia nzima iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Dodoma mwishoni mwa wiki. Umoja huo wa wanawake unaundwa na akina mama kutoka makanisa ya KKKT, Roman Catholics, Anglikana, Moravian na TAC.

Sehemu ya washiriki wa Kongamamo na ibaada ya maombi ya wanawake dunia nzima wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (hayupo pichani) katika Ibaada iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Dodoma mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikabidhi zawadi kwa wachungaji waliohudhuria Kongamamo na ibaada ya maombi ya wanawake dunia katika Wilaya ya Kongwa mwishoni mwa wiki.

Sehemu ya washiriki wa Kongamamo na ibaada ya maombi ya wanawake dunia nzima wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (hayupo pichani) katika Ibaada iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa Katoliki – Wilaya ya Kongwa mwishoni mwa wiki.


UMOJA wa Wanawake wa Madhehebu ya Kikristo Mkoa wa Dodoma hii leo tarehe 3 Machi 2023 umeadhimishi Kongamamo na ibaada ya maombi ya wanawake dunia nzima iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania,  Dayosisi ya Dodoma na katika Viwanja vya Kanisa Katoliki Kongwa.

Akifungua kongamano hilo la maombi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema wanawake ni nguzo katika jamii na chachu ya maendeleo hivyo ni muhimu kwa kundi hili kusimama katika nafasi zao katika kuliombea Taifa, Kanisa na familia ili kuwa kizazi chenye maadili, uzalendo na hofu ya Mungu.

Aidha, Senyamule amewakumbusha jukumu lao kama wanawake na walezi kwa kusisitiza kuwa kila mmoja ana mchango mkubwa katika kufanikisha ustawi katika ngazi ya jamii. “Kumekuwa na  mmonyoko wa maadili katika jamii zetu, kila mmoja ana mchango katika kusimamia maadili na makuzi ya vijana huku tukikemea kwa dhati suala la ukatili wa kijinsia ” alisisitiza Mhe. Senyamule. 

Amewataka akina mama hao kuwa na moyo wa kujiamini, kuthubutu na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali kupitia miradi ya maendeleo na kujiunga katika vikundi ili kunufaika na mikopo inayotolewa na Serikali.

 

Serikali imefanya makubwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya afya kwa lengo la kupunguza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na changamoto za uzazi. Amesema Serikali imetoa kipaumbele katika ujenzi wa Hospitali, Zahanati na ununuzi wa Vifaa na vifaa tiba katika kuimarisha sekta ya afya nchini.

Akizungumzia elimu Mhe. Senyamule amesema Mkoa wa Dodoma umepiga hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu ya elimu kwa kukamilisha ujenzi wa madarasa, vituo shikizi na upatikanaji wa madawati kwa wanafunzi

“Mkoa wa Dodoma tumependelewa katika sekta ya elimu kuna Shule za kutosha, Vyuo vya kati na vile Vikuu, kazi iliyobaki ni kwetu wazazi kuhakikisha watoto wetu wanaenda shule, Serikali imetimiza wajibu wake, na sisi wazazi tutumize wajibu wetu” Amesisitiza Mhe. Senyamule.


Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Fatuma Mganga ametoa rai kwa wanawake wa Dodoma kuwa na malengo mahsusi katika maombi yao ambayo kwayo watajipima mwaka ujao.

“Tuchague mambo ya kuombea na mwaka ujao tuje hapa na shuhuda tukimshukuru Mungu kwa kufanikisha. Tusimame katika nafasi zetu ili tuweze kufanikiwa pia katika kukuza uchumi kwa maendeleo endelevu” Alisisitiza Dkt. Mganga.

Katika kuadhimisha siku hiyo ya maombi, Umoja wa Wanawake Wilaya ya Kongwa umetoa vyakula na zawadi mbalimbali kwa wahitaji. Umoja wa Wanawake wa Madhehebu ya Kikristo Mkoa wa Dodoma unaundwa na akina mama kutoka makanisa ya KKKT, Roman Catholics, Anglikana, Moravian na TAC.

About the author

mzalendoeditor