Featured Kitaifa

WAZIRI CHANA : SERIKALI IMEWEKA MAZINGIRA WEZESHI KWA WAWEKEZAJI SEKTA YA UTALII

Written by mzalendoeditor
Waziri  wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana akizungumza  na  Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA) kwenye mkutano wao wa mwaka ambapo amewapongeza kwa kuwa wazalendo wa kuilinda na kutetea nchi kwa watalii wanaoitembelea Tanzania
Mwenyekiti wa TASOTA, Moustafa Khataw akizungumza kabla hajamkaribisha Waziri wa Maliasili na Utalii,Balozi Dkt.Pindi Chana ambapo  ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wao wa kutangaza uzuri wa Tanzania
Waziri  wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana akikabidhiwa tuzo iliyotolewa na na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA) Moustafa Khataw ikiwa ni kutambua mchango wake katika wa kuhakikisha Wanachama wa TASOTA wanafanya kazi zao katika mazingira wezeshi ikiwemo kero zao kutatuliwa kwa wakati
Waziri  wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kutaka kuwekeza kwenye  sekta ya utalii nchini ili kuweza kutafsiri kwa vitendo maono ya Rais Samia kupitia filamu ya The Royal Tour
Ametoa kauli hiyo jana usiku Jijini Dare s Salaam wakati akizungumza  na  Chama cha Mawakala wa usafiri wa anga Tanzania (TASOTA) kwenye mkutano wao wa mwaka ambapo kila mwaka hukutana mara moja kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu ustawi wa Chama chao.
Amesema  Serikali imepunguza ada ya kila mwaka kwa Mawakala  wa Usafiri wa anga nchini  ( TALA fee )  kutoka dola za Marekani 2,000 hadi dola 500
Pia ameeleza kuwa Serikali imejipanga kupunguza utitiri wa kodi katika sekta ya utalii  ili kuhamasisha Wawekezaji zaidi katika sekta hiyo ili iweze kutoa ajira nyingi zaidi.
Ameongeza kuwa  Serikali imeendelea kuwekeza miundombinu bora katika maeneo ya Hifadhi ikiwemo barabara zenye uwezo wa kupitika muda wote pamoja na usimikaji wa mtandao wa intaneti katika mlima Kilimanjaro. 
Amesisitiza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili kuondoa vikwazo kwa wadau wenye nia ya kutaka kuwekeza hapa nchini.
Akizungumzia umahiri wa  TASOTA, Waziri Chana amesema Wanachama  hao  wamekuwa wazalendo na  Mabalozi wa  kutangaza vivutio vya utalii nchini kwa wageni wanaotaka kuja kujionea uzuri wa Tanzania 
” Najisikia fahari  kuona TASOTA, wakifanya kazi usiku na mchana ya kuilinda na kuitetea taswira ya nchi kwa kuratibu  na kupanga safari za watalii wanaotembelea Tanzania ” 
Aidha, Dkt.Chana ameihaikikishia TASOTA kuwa yeye kama Waziri mwenye dhmama ataendelea kufanya kazi kwa ukaribu na jumuiya hiyo  ili sekta ya utalii iweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Naye Mwenyekiti wa TASOTA, Moustafa Khataw amesema anaishukuru Serikali kwa kutambua mchango wao wa kutangaza uzuri wa Tanzania
” Tumekuwa tukifanya kazi zetu kwa weledi wa hali ya juu katika tasnia hii  ya usafirishaji kwani ni biashara hii  haina njia za mkato wala haina ujanja ujanja inahitaji watu wazalendo  na wenye haiba nzuri katika kuwahudumia watalii wetu ” amesema Mwenyekiti Khataw.

About the author

mzalendoeditor