Uncategorized

WAZIRI MKENDA ATETA NA WAMILIKI WA SHULE BINAFSI JIJINI DODOMA

Written by mzalendoeditor

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,akizungumza wakati wa kikao cha pamoja na wamiliki wa shule binafsi chenye lengo la kujadili na kuboresha masuala mbalimbali ya elimu nchini kilichofanyika leo Januari 21,2023 jijini Dodoma.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,akisisitiza jambo kwa wamiliki wa shule binafsi wakati wa kikao cha pamoja chenye lengo la kujadili na kuboresha masuala mbalimbali ya elimu nchini kilichofanyika leo Januari 21,2023 jijini Dodoma.

 

SEHEMU ya Washiriki wakimsikiliza Waziri  wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda (hayupo pichani) wakati wa kikao cha pamoja na wamiliki wa shule binafsi chenye lengo la kujadili na kuboresha masuala mbalimbali ya elimu nchini kilichofanyika leo Januari 21,2023 jijini Dodoma.

……………………………………….

Na.Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,amewataka wamiliki wa shule binafsi kusimamia malezi kwa wanafunzi katika shule zao ili kuendelea kutoa kizazi chenye maadili mema katika Taifa.

Hayo ameyasema leo Januari 21,2023 jijini Dodoma wakati wa kikao cha pamoja na wamiliki wa shule binafsi ambapo amesema  suala la maadili lazima liangalie na kufanyiwa kazi Kwa ukaribu na umakini mkubwa.

”Wamiliki simamie malezi kwa wanafunzi wetu katika shule zenu  ili kuendelea kutoa kizazi chenye maadili na kuondokana matukio mabaya yanayoripotiwa katika baadhi ya shule kuwa kuna mafundisho yanayotolewa ya tabia chafu.”amesema Prof.Mkenda

Pia  amesema kuwa kuanzia sasa ni lazima vitabu vyote vinavyokuja kutumika mashuleni vikaguliwe kabla havijaaza kutumika ili kuona kama vinakwenda sambamba na maadili ya kitanzania.

“Tunayo maadili yetu ambayo lazima tuyalinda na kuyasimamia yasipotee, hata vitabu vinavyotumika lazima sasa vikaguliwe kabla ya kuanza kutumika ili kuondokana na matumizi ya vitabu ambavyo havina maadili kwa jamii yetu,”amesisitiza 
Hata hivyo Waziri  Mkenda amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na shule binafsi katika kuinua na kuendeleza sekta ya elimu hapa nchini.
“Niwatoe wasiwasi kuwa Serikali inatambua na inathamini mchango wenu katika maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini hivyo msifikirie kwamba tumewaacha nyuma hapana tunawahitaji sana muendelee kuwekeza katika Elimu yetu,”amesema Prof.Mkenda
Pia Waziri Mkenda amesema kuwa  suala la wizi na uvujishaji wa mitihani ni jinai na kutangaza kuwachukulia hatua watendaji, wasimamizi, walimu na wote watakaothibitika kuhusika katika jambo hilo na kusababisha shule binafsi zipatazo 22 kufungiwa vituo vya mitihani.
“Mitihani ni gharama katika shule hizo kulikuwa na wasimamizi wa mitihani, vyombo vya ulinzi na usalama  ikiwemo, watu kutoka taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Polisi, usalama wa Taifa, Baraza la mitihani, labda niwambie tatizo hilo la wizi wa mitihani halipo kwenye shule binafsi pekee lipo hata shule za Serikali,”amesema Mkenda.
Kwa upande wao Wamiliki wa Shule binafsi wamemuomba Prof. Mkenda katika bajeti ya Wizara ijayo kuongeza bajeti ya kuwalipa idara ya Uthibiti Ubora wa Shule wakati wanakwenda kutekeleza jukumu la kukagua shule kwani imekuwa ikiwaumiza kulipa ili waende kukaguliwa.
Pia Wamiliki hao wameomba kuondolewa kwa gharama za Mitihani kwa wanafunzi wanaosoma katika shule binafsi kwani hawana tofauti na wanafunzi wanaosoma shule za Serikali ambao wao wamefutiwa gharama za mitihani.

About the author

mzalendoeditor