Featured Kitaifa

WAZIRI AWESO AAGIZA KUPANGIWA KAZI NYINGINE MENEJA WA RUWASA WILAYA YA  KILOSA

Written by mzalendoeditor
Na Farida Mangube Morogoro.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ameagiza wakala wa maji safi na uasafi wa mazingira vijijini RUWASA kumpangia kazi nyingine Mhandisi wa maji  Wilaya ya Kilosa Joshi Chum baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wake kwenye miradi ya maji.

Waziri Aweso amelazimika kutoa agizo hilo akiwa kwenye ziara yake eneo la Ruaha Mji mdogo wa Mikumi wilaya ya Kilosa mkoani  Morogoro baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na Mbunge wa Jimbo la Mikumi Denis Londo juu ya kero ya kudumu ya maji iliyokuwepo kwa muda mrefu kwenye Kata hiyo.
Alisema Wizara ina nia njema na watendaji wake huku ikiwa na nafasi nyingi hivyo Mhandisi huyo ni vyema akarudi wizarani na mtu mwingine mwenye uwezo wa kufanya kazi na kusimamia miradi apelekwe wilayani Kilosa.
“Lakini kwa dhati ya moyo kabisa pamoja na kazi nzuri anayoifanya,  kwa Ruaha naomba atupishe, Wiraza ya maji ina nafasi nyingi za kufanyakazi  tutakupa nafasi nyingine lakini Kilosa tutamleta mtu ambaye atawasaidia”. Alisema Waziri Aweso. 
Waziri Aweso alisema yeye kabla  ya kuwa Waziri alikuwa Naibu wa Wizira hiyo na kufanya ziara katika Mkoa wa Morogoro Jimboni humo lakini  kilichomsikitisha wataalamu wake hawakuwahi kumpeleka Ruaha hata mara moja.
Hivyo amewataka wahandisi wa maji nchini kuhakikisha wanampeleka kwenye changamoto za maji pindi anapofanya ziara kwenye maeneo yao ya kukagua miradi ya maji ili kutatua changamoto zilipo kwa wananchi.
“ Nionyeshe masikitiko yangu na nitume salamu kwa wahandisi wote nchini, Waziri wa maji anapokuja kukagua miradi mpelekeni kwenye changamoto, ndugu zangu wana Ruaha leo sijaja kuuza sura nimekuja kufanya kazi, elezeni kero zenu wala hamna sababu ya kumuogopa mtu ambaye anakwamisha maendeleo yenu”. Alieleza.
Aweso alisema wakati mwingine wananchi wanakosa maendeleo na kupiga hatua kwasababu ya kuawabeba watu kwa kuwaonea aya na kuwakumbatia wanaowarudisha nyuma, lakini bila ya Mbunge Londo asingefika Ruaha.
Pia  Waziri huyo alitangaza kuvunja jumuiya ya watumiaji maji Kata ya Ruaha huku akiagiza kufanyika uchunguzi kwa jumuiya zote nchini kwa sababu ya kuwepo kwa jumuiya nyingi hewa na zinazowanufaisha viongozi . 
Aidha kutokana na changamoto zilizojitokeza Ruaha Waziri Aweso amemuagiza Mkuu wa Wilaya, Mbunge na wananchi kushirikiana pamoja kupata eneo litakalojengwa ofisi ya Mamlaka ya maji huku akiagiza mfuko wa maji NWF kutenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi huo mara moja.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mikumi Denis Londo alisema pamoja na juhudi za Serikali katika kuhakikisha Jimbo hilo linapata maji amefanikisha kupatikana kwa pampu za maji zenye thamani ya shilingiBil. 1 katika mitaa na vitongozi Kata ya Ruaha na maeneo ya jirani.
Alisema wakati wananchi wakisubiri kukamilika kwa mradi wa maji wa Ruaha wa shilingi Bil.4 unaotekelezwa na Serikali kwa sasa wataweza kupata maji kupitia visima vitakavyochimbwa katika Kata za Kidodi, Luhembe, Masanze, Kizunguzi, Mabwelebwele, Mhenda .
Mmoja wa  wakazi wa Ruaha Neema Makweta alisema ujio huo wa Waziri wa maji umepeleka manufaa kwao kutokana na wananchi kutokuwa na maji ya uhakika huku wakikosa imani na Mhandisi wa RUWASA Wilaya ambaye amekuwa  mdanganyifu wa upatiakanaji wa maji mara kwa mara.
“ kwanza Mhe. Waziri, wamekuwa wakija viongozi wengi na kila mara tumekuwa tukilalamika kuhusu maji na hakuna utekelezaji tunaouna, hatushirikishwi, wanatoa maji mlimani ya kisima wakati maji mazuri yanapatikana Tanecso.”. alisema 
Awali aliyekuwa Mhandisi wa maji RUWASA Wilaya ya Kilosa Joshi Chum akizungumzia mradi wa maji Ruaha alisema umefikia asilimia 30 ya ujenzi wake huku upatikanaji wa maji kwa Wilaya ya Kilosa ukiongezaka kutoka asilimia 73 hadi 78 pindi miradi itakapokamilika.
Nae Mwenyekiti wa UWT Jamila Miyonga alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazozifanya za dipromosia ya siasa na maendeleo ikiwemo kupigania kumtua mama ndoo kichwani.

About the author

mzalendoeditor