MSIMU mpya wa Kampeni ya Samia Nivishe kiatu inayofanywa na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao inatarajia kuanza kutekelezwa katika mikoa ya Lindi,Mtwara,Songea, Iringa pamoja na Visiwani Zanzibar.
Hadi sasa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao chini ya Uongozi mahiri wa Mwenyekiti wake Steven Mengele maarufu kwa jina la Steve Nyerere imeshawavisha wanafunzi wengi viatu kupitia Kampeni ya Samia Nivishe Kiatu 2022 na sasa msimu mpya wa kampeni utaendelea kwenye mikoa hiyo.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steve Nyerere amesema kwamba lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha kila mtoto mwanafunzi mwenye uhitaji anavaa Kiatu cha Samia Suluhu.
“Msimu mpya unaanza Samia nivishe kiatu utafanyika katika Mkoa wa Lindi, Mtwara,Songea Iringa pamoja na Visiwani Zanzibari, kote huko tunataka wanafunzi wavae kiatu cha Samia Suluhu.
“Kiatu cha Samia Suluhu kitavaliwa katika shule mbalimbali nchini na tutapita kwenye shule na kuwakabidhi watoto wenyewe viatu hivyo kwa ajili ya mazingira mazuri ya masomo kwa watoto,”amesema Stive Nyerere alipokuwa akielezea kuanza kwa msimu huo mpya.
Kwa mujibu wa Steve Nyerere Kampeni ya Nivishe Kiatu cha Samia Suluhu itafanyika nchini nzima na kwa sasa wameshipita katika mikoa kadhaa kwa kuanza na Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani na baadae Mkoa wa Tabora.
Aidha ametumia nafasi hiyo kuelezea kubwa tangu kuanza kwa Kampeni hiyo wanashukuru kwa kuungwa mkono na wadau mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine wameifanya Kampeni hiyo kuwa rahisi kwao huku akisisitiza wataendelea nayo hadi wahakikishe wanafunzi wenye uhitaji wa viatu kote nchini wanafikiwa na kuvaa Kiatu cha Samia Suluhu.
Kampeni hiyo ulizinduliwa mwaka 2022 na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao ambayo inaundwa na wasanii wa filamu na muziki Tanzania na kauli mbiu yake ni ‘Samia Nivishe Kiatu 2022’ huku dhumuni kuu likiwa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya elimu.